SERIKALI na wadau mbalimbali wameshauriwa kufanya kazi kwa ushirikiano ili kupunguza athari zitokanazo na mabadiliko ya tabianchi inayoendelea kuongezeka siku hadi siku nchini na duniani kote.
Hayo yalisemwa na Shirika la Maendeleo la Sweden linalopambana na umasikini na kuboresha mazingira (Vi Agroforestry), wakati wa maadhimisho ya Siku ya Mara iliyofanyika juzi, yakilenga kukuza uelewa kuhusu mfumo wa ikolojia katika Hifadhi ya Taifa ya Serengeti na Masaai Mara nchini Kenya.
Taarifa ya shirika hilo iliyotolewa kwa vyombo vya habari ilieleza kuwa kutokana na Mto Mara ambao ni muhimu kwa ikolojia ya hifadhi hizo kuwa hatarini kukauka kutokana na mabadiliko ya tabianchi, suala la uhifadhi wa mazingira halipaswi kupuuzwa.
Ilielezwa kuwa tukio la mwaka huu limewakutanisha wadau kutoka serikalini na mashirika mbalimbali ya uhifadhi kwa kujadili na kukubaliana kuhusu suluhisho litakalosaidia utunzaji wa ikolojia katika hifadhi hizo ambapo kaulimbiu ilikuwa “Mimi, Mto Mara – Simama na mimi/Mimi, Mto Mara – Nitunze nikutunze”.
“Ikolojia na Mara-Serengeti imekuwa ikikabiliwa na changamoto nyingi zinazotishia usimamizi wa rasilimali za asili na anuwai ya uhifadhi wa mazingira.
“Changamoto hizi ni pamoja na uchumi jamii, mazingira, athari za mabadiliko ya tabianchi na sera duni, majibu ya kisheria na mwitikio wa taasisi.
“Jamii inayoishi karibu na mfumo wa ikolojia wa Serengeti kwa muda mrefu imekuwa ikikumbwa na migogoro ya wanyama wa porini. Wengi wamekufa na kupoteza wapendwa wao na mazao yao yameharibiwa, simulizi zao zilitufanya kuchukua hatua, kupitia mradi uliofadhiliwa na Jumuiya ya Ulaya unaofahamika kama ‘Sema’,” ilieleza tarifa hiyo.
Taarifa hiyo iliongeza kuwa mradi wa Sema ni mpango wa uhifadhi wa ikolojia ya Serengeti, unaolenga kusaidia utunzaji wa mazingira kwa kuziwezesha jamii za watu kuishi maisha endelevu na kuongeza ushirikiano wa kikanda.
Mradi huo unatekelezwa katika maeneo yanayoonekana kuwa na kiwango kikubwa cha umasikini na migogoro kati ya wananchi na wanyamapori.
“Kwa kushirikiana na Serikali tumeendeleza mpango wa matumizi ya ardhi na mipango ya usimamizi wa chini ya ardhi na sheria ndogondogo za utekelezaji wa shughuli zetu na kutoa mafunzo kwa wakulima zaidi ya 1,800 kuhusu mipango shirikishi ya utumiaji wa ardhi ili kuanzisha matumizi endelevu ya ardhi.
“Tunaamini panapokuwa miti watu hukua, miti husaidia katika kupunguza athari za mabadiliko ya tabianchi, Kwa hiyo tumeunga mkono jamii kwa kupanda miti zaidi ya 12,000 kando ya Mto Mara na kutoa mafunzo kwa zaidi ya wakulima 2,500 kuhusu kilimo endelevu,” ilieleza taarifa hiyo
Chanzo: Mtanzania Digital
Hakuna maoni:
Chapisha Maoni