Alhamisi, 19 Machi 2020

PATA UFAHAMU KUHUSU CORONA


Hiki ni kirusi cha aina gani?
Corona ni jamii kubwa ya virusi vinavyosababisha maradhi kwa wanyama na binadamu. Kwa binadamu, jamii kadhaa za virusi vya Corona vinafahamika kusababisha maambukizi kwenye njia ya hewa na mfumo wa upumuaji. Maradhi yaliyowahi kusababisha madhara makubwa kutokana na virusi vya Corona ni pamoja na MERS na SARS yaliyozuka mwanzoni mwa miaka ya 2000. Kirusi cha Corona kilichogundulika hivi karibuni kinasababisha ugonjwa unaofahamika kama COVID-19.
COVID-19 ni nini?
COVID-19 ni ugonjwa wa kuambukiza unaosababishwa na virusi vya Corona. Virusi hivyo vipya havikuwa vikifahamika hapo kabla na sayansi ya tiba. Na vilianzia nchini China mwezi Disemba mwaka 2019.
Dalili za Corona ni zipi?
Dalili kuu za Corona ni pamoja na Homa kali, Uchovu na Kikohozi kikavu na zinatokea taratibu. Dalili kubwa na inayoweza kutia hofu, ni mtu kukosa pumzi. Lakini isikutishe, ni mtu 1 pekee kati ya watu 6 walioambukizwa virusi vya Corona hufikia dalili hiyo ya hatari. Na asilimia 80 ya walio na virusi hivyo hupata nafuu bila kuhitaji msaada wa matibabu.
Makundi yaliyo kwenye hatari zaidi ni yapi?
Shirika la Afya Duniani WHO linasema wazee na watu wenye magonjwa ya kudumu kama Shinikizo la Damu, Kisukari, Matatizo ya Figo ndiyo walio kwenye hatari zaidi ya kuathika pindi wanapopatwa na virusi vya Corona. Watu wa umri wa wastani na wenye afya imara wanaweza kupata virusi vya Corona na kupona bila kuhitaji matibabu.
Virusi vya Corona vinasambaa vipi?
Watu wanaweza kupata Virusi vya Corona kutoka kwa watu walioambukizwa. Virusi vinaweza kusambaa kupitia maji maji kutoka kwenye pua au mdomo wa aliyeathirika. Iwapo mtu anagusa maji maji kama mafua, mate na makohozi ya mtu aliye na virusi na kisha kujigusa mdomo, macho na pua anaweza kupata virusi vya Corona.
Ninaweza kujikinga vipi na Virusi vya Corona?
Nawa vizuri na kila wakati mikono yako kwa maji ya vuguvugu, sabuni au dawa za kuua vijijidudu kwa angalau sekunde 20.
Kaa umbali wa angalau hatua mbili (2) kutoka mtu anayepiga chafya au kukohoa.
Epuka kushika macho, pua na mdomo kwa mikono isiyo safi kwa sababu mikono hushika sehemu nyingi na ni rahisi kubeba vimelea vya maradhi.
Hakikisha wewe, na walio karibu yako wanazingatia ustaarabu wa kuzuia pua na mdomo wakati wa kukohoa au kupiga chafya.
Baki nyumbani ikiwa hujisikii vizuri. Iwapo una mafua makali, homa, kikohozi na kushindwa kuhema nenda hospitali kwa sababu huko wataalamu watakupatia msaada muhimu
Epuka kuwa sehemu yenye msongamano, kama vyombo vya usafiri, maduka na maeneo yenye yenye mgandamizo wa hewa.
Nunua kifunika mdomo na pua na kukikavaa ukiwa kwenye mikusanyiko.
Fuatilia taarifa za afya na matangazo yake kuhusu virusi vya Corona.
Kwanini watu wanawekwa karantini?
Kwa ufupi neno Karantini linamaanisha kuwa chini ya uangalizi. Watu wenye dalili au wanaotokea maeneo yenye maambukizi makubwa ya virusi vya Corona hulazimikwa kuwekwa karantini (kutengwa na watu wengine) ili kufuatilia afya yao kwa karibu na kuzuia kueneza virusi. Ukiambiwa unapaswa kuwekwa Karantini, usiogope. Ni kwa ajili ya afya yako na wengine.
Virusi vya Corona vina tiba?
Hadi sasa hakuna tiba au chanjo dhidi ya virusi vya Corona lakini kwa sababu virusi hivyo vinaleta dalili mfano wa zile za mafua makali, mchanganyiko wa tiba unatumika kupunguza athari za virusi vya Corona.
Ninapaswa kuwa na hofu?
Hapana. Hupaswi kuogopa wala kuwa na hofu. Bali unapaswa kuchukua tahadhari. Kila mtu duniani yuko kwenye uwezekano wa kupata virusi vya Corona lakini kama tulivyokufahamisha, athari zake bado hazitishi.
Ni kweli watu weusi hawawezi kupata Corona?
Hapana, kama ilivyo kwa watu wa rangi na jamii zote sisi watu weusi pia tunaweza kuambukizwa virusi vya Corona.

KWA TAARIFA KUHUSU UGONJWA WA COVID 19
PIGA SIMU 
0800 110 124
0800 110 037

Jumanne, 17 Machi 2020

Ugonjwa wa COVID-19. Hatua za tahadhari zilizochukuliwa na ofisi ya Vi Tanzania


Mwezi wa kwanza (January) 2020, Shirika la afya duniani (WHO) lilitangaza mlipuko wa ugonjwa mpya uliojulikana kwa jina la virusi vya corona. Kwa mara ya kwanza ugonjwa umetokea katika jimbo la Hubei nchini China. Shirika la afya duniani limeutangaza ugonjwa huu kuwatishio kwa afya ya jamii kimataifa. Maeneo yote ya jamii yetu,ambayo ni pamoja na biashara na ajira, lazima kuwa mustari wa mbele kama tuna hitaji kudhibiti kuenea kwa ugonjwa huu. Leo jumatatu ya tarehe 16 machi, mgonjwa wa kwanza wa COVID-19 ametambuliwa Tanzania katika mkoa wa Arusha.

Mgonjwa wa COVID-19 anapo kohoa au kupiga chafya hutoa majimaji yenye vimelea vya maambukizi. Majimaji haya hudondoka jirani na pia kwenye vitu kama madawati, meza nahata simu ya mkononi.Watu waliopo jirani wanaweza ambukizwa kwa kugusa vitu hivyo. Hiyo ni baada ya kuwa wamegusa macho yao, pua nahata midomo. Kama utakuwa umesimama ndani umbali wa mita moja kutoka alipo mgonjwa wa COVID-19 unawezaambukizwa kwa njia ya hewa. Kwa maana nyingine ugonjwa wa COVID-19 unaambukizwa sawa na ugonjwa wa mafua.Watu wengi waliougua ugonjwa wa COVID-19 wamekuwa na dalili za kawaida/nyepesi na baadaye kupona.

Ofisi ya Vi Agroforestry Tanzania, inachukua hatua zifuatazo:

*         Ikiwa hujisikii vizuri,hata kama una mafua na kikohozi cha kawaida,au homa ya kawaida, tafadhali baki nyumabani, na kama ikiwezekana fanya kazi zako za kiofisi ukiwa nyumbani.Epuka kugusana na mtu au mwanafamilia alie ndani ya umbali wa mita moja, hii ni kulinda usalama wa wengine ili usiwaambukize. Pia kama unashaka kuambukizwa COVID-19 fika hospitali haraka iwezekanavyo.

*         Nawa mikono yako mara kwa mara kwa kutumia sabuni na maji. Ni kwa sababu kunawa mikono huua virusi vya corona vilivyoko mikononi mwako na kuzuia kuenea kwa ugonjwa wa COVID-19.Kunawa mikono vizuri,tena mara kwa marani njia yenye ufanisi zaidi ya kuzuia kuenea kwa ugonjwa huu,zaidi ya matumizi ya kemikaliza kwa kusafisha mikono. Epuka kugusa macho yako, pua na mdomo kwa mikono isiyo safi.


*         Walakini, sabuni ya kunawa mikono yenye 60% alcohol itakuwepo getini mwa ofisi za Vi Agroforestry, kwa ajili ya wafanyakazi na wageni kunawa mikono yao kabla ya kuingia ofisini. Pia sabuni hizo zitakuwepo ndani ya ofisi.

*         Tutahakikisha mazingira yetu yote yanakuwa safi. Hii ni pamoja na madawati na meza, simuna komputa za mezani. Vyote vita safishwa na kufutwa kwa dawa mara kwa mara.

*         Tutapunguza kutumia usafiri wa umma kwa wafanyakazi,pia kufanya kazi tukiwa majumabani itakuwa njia mbadala. Gari za shirika zitatumika kwa usafiri, kama haitawezekana, safari zisizozalazima zitaahirishwa au kufutwa.

*         Epuka au ahirisha shughuli zinazo husisha watu wengi mfano mikutano na mashirika wenza.

*         Fuatilia mwenendo wa ugonjwa katika maeneo yanayo kuzunguka. Chanzo cha taarifa iwe wizara ya afya au shirika la afya duniani (WHO) kwa anuani hii https://www.who.int/emergencies/diseases/novel-coronavirus-2019 . Usiamini sana taarifa kutoka mitandao ya jamii.


Kent Larsson
Country Manager
~~~~~~~~~~~~~~~~~~~~~~~~
Vi Agroforestry/Vi-Skogen
Country Office Tanzania
P.O. Box 621, Mwanza, Tanzania

Kauli mbiu yetu

BUFADESO kwa maendeleo ya wakulima

MUHIMU

Makala na picha zinazochapishwa katika blogu hii ni kwa ajili ya taarifa na kumbukumbu za Shirika la Bunda Farmers Development Support Organization (BUFADESO)
Hairuhusiwi kutumia yaliyomo katika blogu hii (HASA PICHA) kwa shughuli zozote bila ruhusa ya mmiliki wa blogu hii ambaye ni BUFADESO