Jumatano, 9 Agosti 2017

TAARIFA KUTOKA WIZARA YA AFYA, MAENDELEO YA JAMII, JINSIA, WAZEE NA WATOTO.

TAARIFA KWA UMMA
Msajili wa Mashirika Yasiyo ya Kiserikali anatarajia kuhakiki Mashirika yote Yasiyo ya Kiserikali kuanzia tarehe 21 hadi 31 Agosti, 2017. Lengo kuu la zoezi hili ni Kuhuisha orodha ya Mashirika Yasiyo ya Kiserikali nchini, Kuboresha Kanzi Data ya Mashirika Yasiyo ya Kiserikali na kupima utekelezaji wa majukumu ya Mashirika haya. Zoezi hili litafanyika katika Kanda tano (5). Kanda ya Mashariki itahudumia mikoa ya DAR ES SALAAM, LINDI, MTWARA, PWANI na MOROGORO na Kituo kitakuwa Idara ya Uratibu wa NGOs DAR ES SALAAM; Kanda ya Kati itahudumia mikoa ya DODOMA, SINGIDA, TABORA na KIGOMA na Kituo kitakuwa DODOMA, Makao Makuu wa Wizara ya Afya, Maendeleo ya Jamii, Jinsia, Wazee na Watoto iliyopo Chuo Kikuu cha Dodoma, Kitivo cha Sanaa na Sayansi ya Maendeleo ya Jamii, Jengo Na. 11, Dodoma; Kanda ya Kaskazini itahudumia mikoa ya KILIMANJARO, TANGA, ARUSHA na MANYARA na Kituo kitakuwa katika Ofisi ya Katibu Tawala (M) KILIMANJARO; Kanda ya Ziwa itahudumia mikoa ya MWANZA, KAGERA, MARA, GEITA, SIMIYU na SHINYANGA na Kituo kitakuwa katika Ofisi ya Katibu Tawala (M) MWANZA na Kanda ya Nyanda za Juu - Kusini itahudumia mikoa ya MBEYA, RUVUMA, KATAVI, RUKWA, SONGWE, NJOMBE na IRINGA na Kituo kitakuwa katika Ofisi ya Katibu Tawala (M), MBEYA. Wakati wa uhakiki kila shirika linapaswa kuwasilisha Cheti Halisi cha Usajili, Nakala ya Cheti cha Usajili, kujaza fomu ya uhakiki NGO-Fomu/UHK/2017 inayopatikana katika Tovuti (www.tnnc.go.tz), Stakabadhi za Malipo ya Ada ya mwaka toka kuanzishwa kwa shirika, Barua kutoka kwa Afisa Maendeleo ya Jamii (Mkoa/Wilaya/Halmashauri/Manispaa) ikithibitisha uwepo wa Ofisi ya Shirika na nakala ya katiba iliyothibitishwa na Msajili wa NGOs. Aidha, Mashirika yote yatakayoshindwa kuhakikiwa katika vituo vya Kanda tajwa hapo juu, yatafutiwa Usajili na kuondolewa kwenye Regista ya Msajili wa NGOs. Ili kutoa fursa ya kuhuisha Kanzi Data na Benki ya Takwimu, Usajili wa NGOs utasitishwa kuanzia tarehe 21 Agosti hadi 30 Novemba, 2017.

 M.S. Katemba
MSAJILI WA MASHIRIKA YASIYO YA KISERIKALI

Kauli mbiu yetu

BUFADESO kwa maendeleo ya wakulima

MUHIMU

Makala na picha zinazochapishwa katika blogu hii ni kwa ajili ya taarifa na kumbukumbu za Shirika la Bunda Farmers Development Support Organization (BUFADESO)
Hairuhusiwi kutumia yaliyomo katika blogu hii (HASA PICHA) kwa shughuli zozote bila ruhusa ya mmiliki wa blogu hii ambaye ni BUFADESO