Alhamisi, 16 Mei 2019

Mpango wa Matumizi Bora ya Ardhi


Shirika  la Hifadhi  za  Taifa Tanzania  (TANAPA) kupitia Idara ya  Ujirani Mwema katika Hifadhi ya Taifa Serengeti linashiriki bega kwa bega katika kutekeleza kazi ya Mpango wa Matumizi Bora ya Ardhi unaoendeshwa na Tume ya Taifa ya Mipango ya Matumizi ya  Ardhi  (NLUPC)  kwa  kushirikiana  na  Halmashauri  za  wilaya  ya  Bunda na Tarime  na  Vi Agroforestry   Tanzania.   Kazi   hii   ambayo   imelenga   zaidi   kutekelezwa   katika   vijiji vinavyopakana  na  Hifadhi  ya  Taifa  Serengeti  (SENAPA)  pamoja  na  Pori  la  Akiba  la Grumenti  (GGR)  ilianza  kutekelezwa  katika  Halmashauri  ya  Wilaya  ya  Bunda  20 Novemba, 2018 hadi 08 Aprili, 2019 na inaendelea katika wilaya ya Tarime. Malengo ya kazi hiyo ni:
v  Kupunguza/ kuondoa migogoro ya matumizi ya ardhi kati ya vijiji jirani na Hifadhi za Taifa Tanzania ambayo imekuwa ikijitokeza mara kwa mara
v  Kutoa Elimu ya Uhifadhi, Usimamizi wa rasilimali ardhi na Sheria zinazohusiana na matumizi ya ardhi nchini hususani sheria namba 5 ya ardhi ya vijiji ya mwaka 1999
v  Kutatua migogoro ya ardhi ikiwemo migogoro ya mipaka na uvamizi wa maeneo ya Hifadhi
v  Kuandaa Mipango ya Matumizi ya Ardhi na kurejea Mipango ya Matumizi Bora ya Ardhi ya vijiji iliyopita muda wake
v  Kumilikisha vipande vya ardhi kwa makundi maalum  ya wananchi wasiojiweza, mathalani wazee, wajane na walemavu
v  Kutoa  mapendekezo  ya  namna  ya  kuboresha  hali  za  maisha  kwa  wananchi kupitia  utekelezaji  wa  miradi  mbalimbali  itakayoibuliwa  wakati  wa  kuandaa mipango ya matumizi ya ardhi ya vijiji.

Uendeshaji Mafunzo na Uhamasishaji
1. Vikao vya Uhamasishaji wa Viongozi ngazi ya Wilaya
Uhamasishaji kwa viongozi wa ngazi ya Wilaya pamoja na Waheshimiwa Madiwani juu ya Uandaaji, Usimamizi na Utekelezaji wa Mipango ya Matumizi Bora ya Ardhi katika vijiji ulifanyika  katika  Halmashauri  zote  mbili  (2)  za  Bunda  Wilaya  na  Bunda  Mji.  Aidha, washiriki wa Uhamasishaji wa zoezi hili walikuwa Mkuu wa Wilaya, Kamati ya ulinzi na usalama,  Wakurugenzi  Watendaji  wa  Halmashauri,  Wakuu  wa  Idara  na  Vitengo  na Waheshimiwa  Madiwani  wa  kata  zinazopakana  na  Hifadhi  ya  Taifa  Serengeti.  Pia uhamasishaji   ulihusisha   Maafisa   Tarafa,   Watendaji   Kata,   Watendaji   wa   vijiji   na Wenyeviti wa vijiji vinavyopakana na SENAPA pamoja na GGR.

2. Mafunzo kwa PLUM za Wilaya
Mafunzo kwa ajili ya Kuzijengea uwezo Mamlaka za Upangaji wa Mipango shirikishi ya Matumizi   ya   Bora   ya   Ardhi   za   Halmashauri   za   Wilaya   (Participatory   Land   Use Management Team -  PLUM) yalifanyika. Timu za PLUM za Halmashauri  ya Wilaya ya Bunda na Halmashauri ya Mji wa Bunda zilijengewa uwezo. Mafunzo yaliyotolewa ni:-
v  Sera, Sheria na miongozo mbalimbali ya uandaaji, usimamizi na utekelezaji wa mipango ya matumzi bora ya ardhi
v  Utayarishaji na Utekelezaji wa Mipango ya Matumizi Bora ya Ardhi
v  Matumizi  ya  picha  za  anga  katika  utayarishaji  na  utekelezaji  wa  mipango  ya matumzi ya ardhi ya vijiji
v   Mafunzo  ya  GIS  na  Land  PKS  (kupima  aina  na  uwezo  wa  ardhi  kwa  kuzalisha mazao).

3 Mafunzo kwa Halmashauri za vijiji (VCs), kamati za VLUM na BLAK
 Tangu zoezi hili kuanza mnamo Novemba 20, 2018 hadi kufikia Aprili 04, 2019 jumla ya vijiji 7 vilipatiwa Mafunzo kwa ajili ya kuvijengea uwezo Halmashuri za Vijiji (Mamlaka za Upangaji) na Kamati ya Usimamizi wa Mipango ya Matumizi ya ardhi ya Vijiji (Village Land Use Management - VLUM) pamoja na Mamlaka za utatuzi wa migogoro ya Ardhi vijijini (Baraza la Ardhi la Kijiji – BLAK) wa kuandaa, kusimamia na kutekeleza mipango ya   matumizi   bora   ya   ardhi   pamoja   na   kutatua   migogoroya   Ardhi   vijijini.   Vijiji vilivyopatiwa  mafunzo  hayo  ni  Hunyari,  Kihumbu,  Mariwanda,  Sarakwa,  Mugeta, Kyandege   na   Tingirima   katika   Halmashauri   Wilaya   ya   Bunda.   Pia   kamati   hizo zimefundishwa sheria mbalimbali za Ardhi ikiwa ni pamoja na:
v  Sera ya Ardhi ya mwaka 1995
v  Sheria ya Ardhi Na 4 ya mwaka 1999
v  Sheria ya Ardhi ya vijiji Na 5 ya mwaka 1999
v  Sheria ya uandaaji wa mipango ya matumizi ya Ardhi Na 6 ya 2007
v  Sheria ya mahakama (utatuzi wa migogoro ya Ardhi) Na 2 ya mwaka 2002
v  Sheria Na. 5 ya Uhifadhi Wanyamapori ya mwaka 2009.

Baadhi ya vijiji ambavyo zoezi hili limefanyika ni;   Hunyari, Kihumbu, Sarakwa, Tingirima, Kyandege,  Mugeta, na Mariwanda katika wilaya ya  Bunda.

Jumatano, 20 Machi 2019

MREJEO WA MWELEKEO WA MVUA ZA MASIKA MACHI - MEI 2019

Taarifa hii inatoa mrejeo wa mwelekeo wa mvua za Masika Machi-Mei, 2019

Uwepo wa migandamizo midogo ya hewa kuanzia tarehe 5 Machi, umepelekea kutokea kwa kimbunga (Idai) kuanzia tarehe 10 hadi 15 Machi, 2019 katika rasi ya Msumbiji na kusababisha upepo wenye unyevunyevu kusukumwa kusini mwa Afrika na hivyo kupelekea upungufu wa mvua katika maeneo mengi ya nchi hususan ukanda wa kaskazini. Migandamizo midogo ya hewa inaendelea kujitokeza katika maeneo ya kaskazini mwa Madagascar, ambapo kwa sasa moja ya migandamizo hiyo imeimarika na kuwa kimbunga Savannah. Migandamizo na vimbunga hivi vinatarajiwa kusababisha mvua kuelekea zaidi katika maeneo ya bahari ya Hindi na upungufu katika maeneo mengi ya nchi, kutokana na mahali mwelekeo unaotarajiwa.

Kutokana na mifumo ya hali ya hewa ilivyo kwa sasa na jinsi inavyotarajiwa kuwa kwa kipindi cha Machi – Mei 2019 (kama ilivyoelezwa katika kipengele II cha taarifa hii); 

i. Uwezekano mkubwa wa upungufu wa mvua katika mikoa ya Dar es salaam, Pwani, Tanga, maeneo ya kaskazini mwa mkoa wa Morogoro pamoja na vipindi vichache vya upungufu wa mvua katika maeneo machache ya mikoa ya Kilimanjaro na Manyara.
 ii. Mwelekeo wa mvua za Masika uliotolewa ulionesha kuwa mvua zinatarajiwa kuwa za muda mfupi na kuisha mapema kati ya wiki ya nne ya mwezi Aprili na wiki ya kwanza ya mwezi Mei, 2019. Hata hivyo, hali iliyopo sasa inaonesha uwezekano wa mvua za Masika kuisha mapema zaidi katika baadhi ya maeneo wiki ya pili ya mwezi Aprili, 2019. 
iii. Mvua za msimu (Novemba-Aprili) zinatarajiwa kuendelea kama zilivyotabiriwa. “Mvua za Msimu ambazo zilianza mwezi Novemba, 2018 zinatarajiwa kuendelea hadi mwishoni mwa mwezi April 2019. Katika kipindi hicho mvua hizo za Msimu zinatarajiwa kuwa za wastani katika maeneo mengi. Hata hivyo, mvua za chini ya wastani zinatarajiwa katika maeneo machache ya kanda ya Kusini (Ruvuma), pamoja na mikoa ya Dodoma na Singida”. 

I. MREJEO WA MWELEKEO WA MSIMU WA MVUA KIPINDI CHA MACHI - MEI 2019 
Msimu wa mvua za Masika ni mahususi katika maeneo ya Nyanda za Juu Kaskazinimashariki, pwani ya Kaskazini na visiwa vya Unguja na Pemba, ukanda wa Ziwa Victoria pamoja na kaskazini mwa mkoa wa Kigoma. Ufuatao ni mwelekeo wa mvua za Masika kwa kipindi kilichosalia;

 a) Kanda ya Ziwa Victoria (Mikoa ya Kagera, Geita, Shinyanga, Mwanza, Mara na Simiyu): 
Mvua zinatarajiwa kuwa za wastani kwa ujumla katika maeneo ya mikoa ya Mwanza, Geita, Shinyanga, Simiyu na Mara. Hata hivyo, maeneo machache ya mkoa wa Kagera na wilaya ya Kibondo yanatarajiwa kuwa na upungufu wa mvua. Mvua zinatarajiwa kuisha mapema katika wiki ya tatu ya mwezi Aprili, 2019.

b) Ukanda wa Pwani ya Kaskazini: (Mikoa ya Dar es Salaam, Tanga, Pwani, Visiwa vya Unguja na Pemba pamoja na kaskazini mwa mkoa wa Morogoro):
Katika kipindi cha msimu kilichosalia, mvua za wastani hadi chini ya wastani zinatarajiwa katika maeneo ya mikoa ya Dar es Salaam, Pwani, Tanga pamoja na maeneo ya kaskazini mwa mkoa wa Morogoro. Aidha, mvua za wastani kwa ujumla zinatarajiwa katika maeneo mengi ya visiwa vya Unguja na Pemba. Pamoja na mvua za juu ya wastani kujitokeza katika maeneo machache ya visiwa vya Unguja na Pemba, mvua zinatarajiwa kuisha katika wiki ya nne ya mwezi Aprili, 2019. Mvua katika maeneo ya mikoa ya Tanga, Dar es Salaam, Pwani na maeneo ya kaskazini mwa mkoa wa Morogoro zinatarajiwa kuisha katika wiki ya pili ya mwezi Aprili, 2019. 

c) Nyanda za juu Kaskazini Mashariki: (Mikoa ya Kilimanjaro, Arusha na Manyara): 
Kwa ujumla, mvua za wastani zinatarajiwa katika maeneo mengi. Hata hivyo, mvua za juu ya wastani zinatarajiwa kujitokeza katika maeneo machache ya mkoa wa Arusha. Mvua zinatarajiwa kuisha mapema katika wiki ya tatu ya mwezi Aprili, 2019. 

II. MIFUMO YA HALI YA HEWA 
Hali ya joto la bahari pamoja na mifumo ya hali ya hewa inaonesha upungufu wa mvua katika maeneo mengi yanayopata misimu miwili ya mvua kwa mwaka. Katika kipindi cha msimu kilichosalia, joto la bahari la juu ya wastani linatarajiwa katika maeneo ya kati na kusini magharibi mwa bahari ya Hindi, hali ambayo inatarajiwa kupelekea kuvuma kwa upepo hafifu kutoka mashariki na kusababisha upungufu wa mvua katika maeneo mengi nchini. Halikadhalika, joto la bahari la wastani hadi juu kidogo ya wastani linatarajiwa katika eneo la kusini mashariki mwa bahari ya Atlantic karibu na pwani ya Angola. Hali hii inatarajiwa kupunguza msukumo wa upepo kutoka magharibi na hivyo kupunguza uwepo wa unyevunyevu kutoka misitu ya Kongo. 

III. USHAURI 
Mamlaka ya Hali ya Hewa inawashauri watumiaji wa taarifa za hali ya hewa ikiwa ni pamoja na wakulima, wafugaji, Mamlaka za Wanyamapori, Mamlaka za Maji na Afya waendelee kutafuta, kupata na kufuata ushauri wa wataalamu katika sekta husika. 

Mwelekeo wa mvua uliotolewa hapa umezingatia zaidi kipindi cha msimu (miezi mitatu) na hali ya mvua katika maeneo makubwa. Hivyo, viashiria vinavyochangia mwenendo wa mifumo ya mvua na mabadiliko ya muda mfupi katika maeneo madogo utazingatiwa katika uchambuzi wa utabiri wa muda wa kati na mfupi. Watumiaji wa taarifa za utabiri huu wanashauriwa pia kufuatilia utabiri wa saa 24, siku 10 pamoja na mwezi kama unavyotolewa na Mamlaka ya hali ya Hewa Tanzania. 

Mamlaka ya hali ya hewa Tanzania itaendelea kufuatilia mwenendo wa mifumo ya hali ya hewa na kutoa taarifa za mwelekeo wa mvua nchini. 

Imetolewa na Mamlaka ya Hali ya Hewa Tanzania: 

Dkt. Agnes L. Kijazi 
MKURUGENZI MKUU 
TMA
20 Machi, 2019


Chanzo: tovuti ya TMA

Ijumaa, 8 Machi 2019

SIKU YA WANAWAKE DUNIANI

"BADIRI FIKRA KUFIKIA USAWA WA KIJINSIA KWA MAENDELEO ENDELEVU"
Image may contain: one or more people and crowd
Katika Picha, Mkuu wa Wilaya ya Bunda, Mwl. Lydia S. Bupilipili akikagua shughuli za kijasiriamali zinazofanywa na wanawake wa wilaya ya Bunda. Kauli mbiu ya mwaka huu kitaifa inalenga kubadiri fikra kwa wanajamii ili waweze kumthamini mwanamke kuwa anaweza kufanya kama mwanaume. Hivyo basi jamii inasisitizwa kuzingatia usawa wa kijinsia kuanzia fursa, matumizi ya rasilimali na muda. Tukiwapa wanawake na wanaume fursa sawa, itakuwa chachu kubwa ya kufikia maendeleo endelevu.

Na:
Baraka Kamese

Kauli mbiu yetu

BUFADESO kwa maendeleo ya wakulima

MUHIMU

Makala na picha zinazochapishwa katika blogu hii ni kwa ajili ya taarifa na kumbukumbu za Shirika la Bunda Farmers Development Support Organization (BUFADESO)
Hairuhusiwi kutumia yaliyomo katika blogu hii (HASA PICHA) kwa shughuli zozote bila ruhusa ya mmiliki wa blogu hii ambaye ni BUFADESO