Alhamisi, 11 Julai 2019
Alhamisi, 16 Mei 2019
Mpango wa Matumizi Bora ya Ardhi
Shirika la Hifadhi
za Taifa Tanzania (TANAPA) kupitia Idara ya Ujirani Mwema
katika Hifadhi ya Taifa Serengeti linashiriki bega kwa bega katika kutekeleza
kazi ya Mpango wa Matumizi Bora ya Ardhi unaoendeshwa na Tume ya Taifa ya
Mipango ya Matumizi ya Ardhi (NLUPC) kwa
kushirikiana na Halmashauri za wilaya ya
Bunda na Tarime na Vi Agroforestry
Tanzania. Kazi hii ambayo
imelenga zaidi kutekelezwa
katika vijiji vinavyopakana na Hifadhi ya
Taifa Serengeti (SENAPA) pamoja na Pori
la Akiba la Grumenti (GGR) ilianza
kutekelezwa katika Halmashauri ya Wilaya ya
Bunda 20 Novemba, 2018 hadi 08 Aprili, 2019 na inaendelea katika wilaya ya
Tarime. Malengo ya kazi hiyo ni:
v Kupunguza/ kuondoa
migogoro ya matumizi ya ardhi kati ya vijiji jirani na Hifadhi za Taifa
Tanzania ambayo imekuwa ikijitokeza mara kwa mara
v Kutoa Elimu ya
Uhifadhi, Usimamizi wa rasilimali ardhi na Sheria zinazohusiana na matumizi ya
ardhi nchini hususani sheria namba 5 ya ardhi ya vijiji ya mwaka 1999
v Kutatua migogoro
ya ardhi ikiwemo migogoro ya mipaka na uvamizi wa maeneo ya Hifadhi
v Kuandaa Mipango ya
Matumizi ya Ardhi na kurejea Mipango ya Matumizi Bora ya Ardhi ya vijiji
iliyopita muda wake
v Kumilikisha
vipande vya ardhi kwa makundi maalum ya wananchi wasiojiweza, mathalani
wazee, wajane na walemavu
v Kutoa
mapendekezo ya namna ya kuboresha hali
za maisha kwa wananchi kupitia utekelezaji
wa miradi mbalimbali itakayoibuliwa wakati
wa kuandaa mipango ya matumizi ya ardhi ya vijiji.
Uendeshaji Mafunzo na Uhamasishaji
1. Vikao vya Uhamasishaji wa
Viongozi ngazi ya Wilaya
Uhamasishaji kwa
viongozi wa ngazi ya Wilaya pamoja na Waheshimiwa Madiwani juu ya Uandaaji,
Usimamizi na Utekelezaji wa Mipango ya Matumizi Bora ya Ardhi katika vijiji
ulifanyika katika Halmashauri zote mbili
(2) za Bunda Wilaya na Bunda Mji.
Aidha, washiriki wa Uhamasishaji wa zoezi hili walikuwa Mkuu wa Wilaya, Kamati
ya ulinzi na usalama, Wakurugenzi Watendaji wa
Halmashauri, Wakuu wa Idara na Vitengo na
Waheshimiwa Madiwani wa kata zinazopakana
na Hifadhi ya Taifa Serengeti. Pia
uhamasishaji ulihusisha Maafisa
Tarafa, Watendaji Kata,
Watendaji wa vijiji na Wenyeviti wa vijiji
vinavyopakana na SENAPA pamoja na GGR.
2. Mafunzo kwa PLUM za Wilaya
Mafunzo kwa ajili ya Kuzijengea
uwezo Mamlaka za Upangaji wa Mipango shirikishi ya Matumizi
ya Bora ya Ardhi za
Halmashauri za Wilaya
(Participatory Land Use Management Team - PLUM)
yalifanyika. Timu za PLUM za Halmashauri ya Wilaya ya Bunda na
Halmashauri ya Mji wa Bunda zilijengewa uwezo. Mafunzo yaliyotolewa ni:-
v Sera, Sheria na
miongozo mbalimbali ya uandaaji, usimamizi na utekelezaji wa mipango ya matumzi
bora ya ardhi
v Utayarishaji na
Utekelezaji wa Mipango ya Matumizi Bora ya Ardhi
v Matumizi
ya picha za anga katika utayarishaji
na utekelezaji wa mipango ya matumzi ya ardhi ya vijiji
v Mafunzo ya
GIS na Land PKS (kupima aina na
uwezo wa ardhi kwa kuzalisha mazao).
3 Mafunzo kwa Halmashauri za vijiji
(VCs), kamati za VLUM na BLAK
Tangu zoezi hili
kuanza mnamo Novemba 20, 2018 hadi kufikia Aprili 04, 2019 jumla ya vijiji 7 vilipatiwa
Mafunzo kwa ajili ya kuvijengea uwezo Halmashuri za Vijiji (Mamlaka za
Upangaji) na Kamati ya Usimamizi wa Mipango ya Matumizi ya ardhi ya Vijiji
(Village Land Use Management - VLUM) pamoja na Mamlaka za utatuzi wa migogoro
ya Ardhi vijijini (Baraza la Ardhi la Kijiji – BLAK) wa kuandaa, kusimamia na
kutekeleza mipango ya matumizi bora
ya ardhi pamoja na
kutatua migogoroya Ardhi
vijijini. Vijiji vilivyopatiwa mafunzo hayo ni
Hunyari, Kihumbu, Mariwanda, Sarakwa, Mugeta,
Kyandege na Tingirima katika
Halmashauri Wilaya ya Bunda.
Pia kamati hizo zimefundishwa sheria mbalimbali za
Ardhi ikiwa ni pamoja na:
v
Sera ya Ardhi ya mwaka 1995
v
Sheria ya Ardhi Na 4 ya mwaka 1999
v
Sheria ya Ardhi ya vijiji Na 5 ya mwaka 1999
v
Sheria ya uandaaji wa mipango ya matumizi ya Ardhi Na 6 ya 2007
v
Sheria ya mahakama (utatuzi wa migogoro ya Ardhi) Na 2 ya mwaka
2002
v
Sheria Na. 5 ya Uhifadhi Wanyamapori ya mwaka 2009.
Baadhi ya vijiji ambavyo zoezi hili limefanyika ni;
Hunyari, Kihumbu, Sarakwa, Tingirima, Kyandege, Mugeta, na Mariwanda
katika wilaya ya Bunda.
Jumatano, 20 Machi 2019
MREJEO WA MWELEKEO WA MVUA ZA MASIKA MACHI - MEI 2019
Taarifa hii inatoa mrejeo wa mwelekeo wa mvua za Masika Machi-Mei, 2019
Uwepo wa migandamizo midogo ya hewa kuanzia tarehe 5 Machi, umepelekea
kutokea kwa kimbunga (Idai) kuanzia tarehe 10 hadi 15 Machi, 2019 katika rasi ya
Msumbiji na kusababisha upepo wenye unyevunyevu kusukumwa kusini mwa Afrika
na hivyo kupelekea upungufu wa mvua katika maeneo mengi ya nchi hususan ukanda
wa kaskazini. Migandamizo midogo ya hewa inaendelea kujitokeza katika maeneo ya
kaskazini mwa Madagascar, ambapo kwa sasa moja ya migandamizo hiyo imeimarika
na kuwa kimbunga Savannah. Migandamizo na vimbunga hivi vinatarajiwa
kusababisha mvua kuelekea zaidi katika maeneo ya bahari ya Hindi na upungufu
katika maeneo mengi ya nchi, kutokana na mahali mwelekeo unaotarajiwa.
Kutokana na mifumo ya hali ya hewa ilivyo kwa sasa na jinsi inavyotarajiwa kuwa kwa
kipindi cha Machi – Mei 2019 (kama ilivyoelezwa katika kipengele II cha taarifa hii);
i. Uwezekano mkubwa wa upungufu wa mvua katika mikoa ya Dar es salaam,
Pwani, Tanga, maeneo ya kaskazini mwa mkoa wa Morogoro pamoja na vipindi
vichache vya upungufu wa mvua katika maeneo machache ya mikoa ya
Kilimanjaro na Manyara.
ii. Mwelekeo wa mvua za Masika uliotolewa ulionesha kuwa mvua zinatarajiwa
kuwa za muda mfupi na kuisha mapema kati ya wiki ya nne ya mwezi Aprili na
wiki ya kwanza ya mwezi Mei, 2019. Hata hivyo, hali iliyopo sasa inaonesha
uwezekano wa mvua za Masika kuisha mapema zaidi katika baadhi ya maeneo
wiki ya pili ya mwezi Aprili, 2019.
iii. Mvua za msimu (Novemba-Aprili) zinatarajiwa kuendelea kama zilivyotabiriwa.
“Mvua za Msimu ambazo zilianza mwezi Novemba, 2018 zinatarajiwa
kuendelea hadi mwishoni mwa mwezi April 2019. Katika kipindi hicho mvua
hizo za Msimu zinatarajiwa kuwa za wastani katika maeneo mengi. Hata hivyo,
mvua za chini ya wastani zinatarajiwa katika maeneo machache ya kanda ya
Kusini (Ruvuma), pamoja na mikoa ya Dodoma na Singida”.
I. MREJEO WA MWELEKEO WA MSIMU WA MVUA KIPINDI CHA MACHI -
MEI 2019
Msimu wa mvua za Masika ni mahususi katika maeneo ya Nyanda za Juu Kaskazinimashariki, pwani ya Kaskazini na visiwa vya Unguja na Pemba, ukanda wa Ziwa
Victoria pamoja na kaskazini mwa mkoa wa Kigoma. Ufuatao ni mwelekeo wa mvua za
Masika kwa kipindi kilichosalia;
a) Kanda ya Ziwa Victoria (Mikoa ya Kagera, Geita, Shinyanga, Mwanza, Mara
na Simiyu):
Mvua zinatarajiwa kuwa za wastani kwa ujumla katika maeneo ya
mikoa ya Mwanza, Geita, Shinyanga, Simiyu na Mara. Hata hivyo, maeneo
machache ya mkoa wa Kagera na wilaya ya Kibondo yanatarajiwa kuwa na
upungufu wa mvua. Mvua zinatarajiwa kuisha mapema katika wiki ya tatu ya
mwezi Aprili, 2019.
b) Ukanda wa Pwani ya Kaskazini: (Mikoa ya Dar es Salaam, Tanga, Pwani,
Visiwa vya Unguja na Pemba pamoja na kaskazini mwa mkoa wa Morogoro):
Katika kipindi cha msimu kilichosalia, mvua za wastani hadi chini ya wastani
zinatarajiwa katika maeneo ya mikoa ya Dar es Salaam, Pwani, Tanga pamoja na
maeneo ya kaskazini mwa mkoa wa Morogoro. Aidha, mvua za wastani kwa
ujumla zinatarajiwa katika maeneo mengi ya visiwa vya Unguja na Pemba.
Pamoja na mvua za juu ya wastani kujitokeza katika maeneo machache ya visiwa
vya Unguja na Pemba, mvua zinatarajiwa kuisha katika wiki ya nne ya mwezi
Aprili, 2019. Mvua katika maeneo ya mikoa ya Tanga, Dar es Salaam, Pwani na
maeneo ya kaskazini mwa mkoa wa Morogoro zinatarajiwa kuisha katika wiki
ya pili ya mwezi Aprili, 2019.
c) Nyanda za juu Kaskazini Mashariki: (Mikoa ya Kilimanjaro, Arusha na
Manyara):
Kwa ujumla, mvua za wastani zinatarajiwa katika maeneo mengi. Hata hivyo,
mvua za juu ya wastani zinatarajiwa kujitokeza katika maeneo machache ya
mkoa wa Arusha. Mvua zinatarajiwa kuisha mapema katika wiki ya tatu ya
mwezi Aprili, 2019.
II. MIFUMO YA HALI YA HEWA
Hali ya joto la bahari pamoja na mifumo ya hali ya hewa inaonesha upungufu wa mvua
katika maeneo mengi yanayopata misimu miwili ya mvua kwa mwaka. Katika kipindi
cha msimu kilichosalia, joto la bahari la juu ya wastani linatarajiwa katika maeneo ya
kati na kusini magharibi mwa bahari ya Hindi, hali ambayo inatarajiwa kupelekea
kuvuma kwa upepo hafifu kutoka mashariki na kusababisha upungufu wa mvua
katika maeneo mengi nchini. Halikadhalika, joto la bahari la wastani hadi juu kidogo ya
wastani linatarajiwa katika eneo la kusini mashariki mwa bahari ya Atlantic karibu na
pwani ya Angola. Hali hii inatarajiwa kupunguza msukumo wa upepo kutoka
magharibi na hivyo kupunguza uwepo wa unyevunyevu kutoka misitu ya Kongo.
III. USHAURI
Mamlaka ya Hali ya Hewa inawashauri watumiaji wa taarifa za hali ya hewa ikiwa ni pamoja
na wakulima, wafugaji, Mamlaka za Wanyamapori, Mamlaka za Maji na Afya waendelee
kutafuta, kupata na kufuata ushauri wa wataalamu katika sekta husika.
Mwelekeo wa mvua uliotolewa hapa umezingatia zaidi kipindi cha msimu (miezi
mitatu) na hali ya mvua katika maeneo makubwa. Hivyo, viashiria vinavyochangia
mwenendo wa mifumo ya mvua na mabadiliko ya muda mfupi katika maeneo madogo
utazingatiwa katika uchambuzi wa utabiri wa muda wa kati na mfupi. Watumiaji wa
taarifa za utabiri huu wanashauriwa pia kufuatilia utabiri wa saa 24, siku 10 pamoja
na mwezi kama unavyotolewa na Mamlaka ya hali ya Hewa Tanzania.
Mamlaka ya hali ya hewa Tanzania itaendelea kufuatilia mwenendo wa mifumo ya
hali ya hewa na kutoa taarifa za mwelekeo wa mvua nchini.
Imetolewa na Mamlaka ya Hali ya Hewa Tanzania:
Dkt. Agnes L. Kijazi
MKURUGENZI MKUU
TMA
TMA
20 Machi, 2019
Chanzo: tovuti ya TMA
Chanzo: tovuti ya TMA
Jisajili kwenye:
Machapisho (Atom)
Kauli mbiu yetu
BUFADESO kwa maendeleo ya wakulima
MUHIMU
Makala na picha zinazochapishwa katika blogu hii ni kwa ajili ya taarifa na kumbukumbu za Shirika la Bunda Farmers Development Support Organization (BUFADESO)
Hairuhusiwi kutumia yaliyomo katika blogu hii (HASA PICHA) kwa shughuli zozote bila ruhusa ya mmiliki wa blogu hii ambaye ni BUFADESO

