Jumapili, 24 Septemba 2017

UZINDUZI MRADI WA KUHAMASISHA JINSIA KUPITIA NYIMBO ZA ASILI TAR 22/9/2017


 BUFADESO inatekeleza mradi wa kuhamasisha jamii kuhusu usawa wa jinsia, ambapo wanachama vikundi walipewa fursa ya Kuandaa Nyimbo zenye ujumbe unao hamasisha usawa wa jinsia na kupinga ukatili dhidi ya wanawake na mabinti kuanzia ngazi ya familia hadi katika jamii. Ni wazi kuwa jamii yetu ya wilaya ya Bunda inakabiliwa na changamoto ya vitendo vya unyanyasaji wa jinsia na ukatili dhidi ya wanawake na watoto wa kike. Aidha kutoka na Utamaduni na mila za Makabila mengi ya Mkoa wa Mara, jinsia ya kike imekuwa ikinyanyasika kutokana na matendo kandamizi kama kukeketwa, vipigo kwa wake katika familia, matusi na masimango, watoto wa kike kutopewa kipaumblele cha kupelekwa shule, na kuozwa katika umri mdogo, kunyimwa fursa za umiliki wa rasilimali kama ardhi na mashamba, umiliki wa mali kama nyumba na mifugo mikubwa ikiwemo ng`ombe, wanawake wajane kunyimwa mirathi baada ya waume zao Kufariki na matendo mengine ya kumnyima haki mwanamke kama ushiriki wa masuala mbalimbali ya kijamii. Matendo mengine wanayofanyiwa wanawake yana hatarisha afya zao na muda mwingine hupelekea wanawake kuumizwa, kupewa majeraha au ulemavu na wakati mwingine kusababisha vifo kwa wanawake na kitendo ambacho kinaharibu taifa cha kuwapa watoto wa shule mimba.
Wadau mbalimbali wakifatilia ujumbe uliotolewa katika shughuli ya uhamasishaji wa mradi wa uswa wa jinsia.

Kwa kutambua harakati za serikali katika kushughulikia kumaliza changamoto hii inayokabili jamii zetu ya kutokuwa na usawa wa jinsia na unyanyasaji wa wanawake na wasichana, shirika letu linaunga mkono mapambano hayo na kukemea vitendo vyote vinavyohusiana na kumdhalilisha mwanamke.

Maafisa wa idara za Halmashauri za Wilaya na Mji Bunda kstiks uzinduzi huo

Tunaamini burudani ni njia mojawapo ya kufikishwa ujumbe katika jamii, hivyo kupitia burudani BUFADESO imeona fursa ya Kuelimisha na kuhamasisha jamii juu ya Usawa wa jinsia na kupinga ukatili wa jinsia. Tunaamini kupitia mradi huu unao zinduliwa leo, jamii itapata fursa sio tu kuburudika kupitia burudani zilizo andaliwa bali kupata ujumbe na mwisho wa siku kubadirika na kuacha matendo yanayokiuka utu wa mwanamke. Vikundi wanachama wa BUFADESO vimeandaa Nyimbo na ngoma za kiutamaduni au kikabila zenye ujumbe nzuri unaohamasisha usawa wa jinsia. Nyimbo hizo zinajumuisha Nyimbo za kabila la Wakurya maarufu kama Litungu. Nyimbo za kabila la Waikizu zijulikanazo kama Ndono, Kesa na Bwenga. Nyimbo za Wasukuma Masaligula na Kadumu pamoja na kwaya zenye maudhui ya usawa wa jinsia.
Baada ya Uzinduzi huu, BUFADESO itazunguka katika kata 11 za wilaya ya Bunda tunapofanyia kazi ili kuendeleza kuhamasisha jamii juu ya Usawa wa Jinsia. Pamoja na kuzunguka katika maeneo hayo tofauti, tunaomba ushirikiano wa vyombo vya habari katika kutumia Nyimbo na ngoma hizi zilizo andaliwa ili kuhamasisha jamii juu ya jambo hili. Pia tunaomba serikali iendelee kutia mkazo na kutumia sheria juu ya wananchi wanaoendeleza matendo ya unyanyasaji wa jinsia. Mbali na hayo tuna waasa Wanajamii kutoa taarifa kwenye vyombo husika pale wanapofanyiwa au kuona mwananchi anafanya matendo ya unyanyasaji wa jinsia.

Mwisho kabisa tunaomba na kutoa hamasa kwa jamii hasa watu waliopo vijiji tofauti vya wilaya hii ya Bunda kuacha matendo yote yanayo husiana na kunyanyasa na kukandamiza wanawake na hivyo kusababisha wilaya yetu na mkoa wa Mara kwa ujumla kuwa maarufu kwa sifa mbaya ya Unyanyasaji wa Wanawake. BUFADESO tunaamini kuwa katika familia na jamii yoyote haiwezi kupata maendeleo endapo hakuna ushiriki wa wanawake. Bila ushiriki wa wanawake kuanzia ngazi ya familia shughuli hazitafanyika kwa weledi. Wakulima hawawezi kunufaika na kilimo iwapo mwanamke hapewi fursa ya kushiriki katika shughuli za kutoa maamuzi na mawazo ya kuendeleza kilimo cha familia, hiyo pia haiwezekani katika shughuli za kibiashara, hata katika nyanja ya uongozi; haiwezekani kuwa na ufanisi endapo mwanamke atanyimwa fursa na haki zote anazo stahiki. 

Akizindua mradi huu, Mkuu wa Wilaya ya Bunda Mwl Lydia Bupilipili ameilezea jamii kuwa yeye ni mdau mkubwa wa kupinga ukatili wa jinsia. Aidha aliwaasa wananchi kuachana na "mambo ya kale" ya kunyanyasana kwani ni mambo yaliyopitwa na wakati na husababisha kudolola kwa uchumi. Mkuu huyo wa wilaya aliwasisitiza wanacnhi kuachana na mfumo dume na kufanya kazi kwa pamoja. Zaidi aligusia pande zote kuwa wanaonyanyaswa kijinsia sio tu wanawake bali pia wapo wanaume wanaoyanyasika kijinsia na wake zao. Mkuu wa wilaya hii ya Bunda alilipongeza shirika la BUFADESO kwa utekelezaji mzuri wa shughuli zake ikiwemo ya kuhamasisha jamii juu ya usawa wa jinsia.
Mkuu wa wilaya Mwl. Lydia Bupilipili akiongea katika uzinduzi wa mradi wa jinsia, kushoto kwake ni Mwenyekiti wa Halmashauri ya Wilaya Bunda, Bw. Isaack M. Kabugu na kulia kwake Mwenyekiti wa BUFADESO Edward Chacha
Mwl Lydia aligusa zaidi juu ya shughuli za kilimo kwa wanajamii wa wilaya ya Bunda kwani uchumi wa wilaya hii unategemea zaidi kilimo hasa zao la zao. Mkuu huyu wa wilaya aliwaasa wakulima kurudi kulienzi zao la pamba kwani serikali imeweka mpango mzuri wa kuhakikisha wakulima wanalima kwa tija na kunufaika na kilimo cha zao hilo. aliongezea kuwa serikali imeweka mikakati imara ya zao hilo kuanzia pembejeo hadi mauzo.
Mkuu wa wilaya na viongozi wa BUFADESO wakifurahia burudani na ujumbe kutoka ngoma za kikabila

Hakuna maoni:

Chapisha Maoni

Kauli mbiu yetu

BUFADESO kwa maendeleo ya wakulima

MUHIMU

Makala na picha zinazochapishwa katika blogu hii ni kwa ajili ya taarifa na kumbukumbu za Shirika la Bunda Farmers Development Support Organization (BUFADESO)
Hairuhusiwi kutumia yaliyomo katika blogu hii (HASA PICHA) kwa shughuli zozote bila ruhusa ya mmiliki wa blogu hii ambaye ni BUFADESO