Jumatano, 3 Juni 2020

SIKU YA MAZINGIRA DUNIANI 2020


Siku ya Mazingira Duniani huadhimishwa kila tarehe 5 ya mwezi wa sita. Mwaka huu inaadhimishwa Siku ya Ijumaa, tarehe 5 Juni 2020 nchini Colombia. Dhima ya Siku ya Mazingira Duniani mwaka huu italenga "Bioanuai" ambapo kauli mbiu ya mwaka huu inasema "CELEBRATE BIODIVERSITY" kwa tafsiri rahisi "SHEREHEKEA BIOANUAI". Progamu ya Mazingira ya Umoja wa Mataifa; UNEP (UN Environmental Programme) imetangaza kuwa Colombia itakuwa mwenyeji wa Siku ya Mazingira Duniani Mwaka huu kwa kushirikiana na Ujerumani. Siku ya mazingira duniani huadhimishwa na nchi zaidi ya 143, Tanzania ikiwemo. Siku hii pia huitwa "Siku ya Watu"; kuonesha jinsi watu wanavyojali dunia na kusaidia utunzaji wa mazingira ya dunia.

Kwa nini Kauli Mbiu ya Mwaka huu inasema "SHEREHEKEA BIOANUANI" na kwa nini COLOMBIA awe mwenyeji wa mwaka huu?

Kwanza kabisa ni vizuri tukajua maana ya neno Bioanuai

Bioanuani ni mchanganyiko na uwiano wa viumbe hai; wanyama na mimea; vinavyoishi duniani. Bio maana yake ni maisha, na anuwai ni aina, kwa hiyo, bioanuwai ina maana ya aina ya maisha. Inajumuisha vitu vyote vinavyoishi duniani na katika bahari, kuanzia nyangumi wakubwa kabisa mpaka bacteria wadogo kabisa. Mahali ambapo aina nyingi tofauti, au ‘spishi’, au vitu vyenye uhai hukua pamoja, kama vile mwamba wa matumbawe au msitu, panasemekana kuwa na bioanuwai nyingi, na mahali ambapo pana spishi chache, kama shamba lililolimwa, au maeneo ya mjini, pana bioanuwai wachache.


Kauli mbiu inasema tusheherekee bioanui kwa sababu duniani kuna zaidi ya spishi za wanyama na mimea zaidi ya milioni moja. Lakini kutokana na changamoto za kidunia zilizopo sasa, kuna matishio makubwa ya viumbe mbalimbali kutoweka duniani imeonekana kwa sasa una umuhimu zaidi kutilia mkazo katika kulinda bioanuai. Nchi ya Colombia imechaguliwa kuwa mwenyeji wa mwaka huu wa maadhimisho ya Siku ya Mazingira duniani kutokana na uwepo wa wanyama na mimea kwa wingi zaidi katika nchi hii. Nchi ya Colombia ina zaidi ya 10% ya bioanuani zilizopo duniani. Kitakwimu, nchi hiyo ndio inayoongoza (nchi ya kwanza) kwa kuwa aina nyingi ya ndege na pia ni nchi ya pili kwa kuwa na aina nyingi za mimea mbalimbali, vipepeo na samaki wa maji baridi. Pia nchi ya Colombia ni sehemu ya msitu mkubwa duniani uitwao Msitu wa Amazon.

Imeandaliwa na
Baraka Kamese
Mratibu BUFADESO

Kauli mbiu yetu

BUFADESO kwa maendeleo ya wakulima

MUHIMU

Makala na picha zinazochapishwa katika blogu hii ni kwa ajili ya taarifa na kumbukumbu za Shirika la Bunda Farmers Development Support Organization (BUFADESO)
Hairuhusiwi kutumia yaliyomo katika blogu hii (HASA PICHA) kwa shughuli zozote bila ruhusa ya mmiliki wa blogu hii ambaye ni BUFADESO