Jumatatu, 18 Januari 2016

TUJIUNGE NA VIKUNDI VYA HISA

Vikundi vya Hisa (kuweka na kukopa) ni mpango uliosaidia na unaoendelea kusaidia maisha ya wakulima vijijini kupata fursa ya kujiwekea akiba na kupata mikopo yenye masharti nafuu. Mpango huu umesaidia kuinua maisha ya wakulima hasa kupata mitaji ya kuanzisha na/au kuendeleza shughuli za kilimo na ufugaji pamoja na biashara ndogondogo.
                                                                                 Wanachama wa kikundi cha Hisa kutoka kijiji cha Sarawe wilayani Bunda

Vikundi vya Hisa ni vikundi gani?
Hivi ni vikundi vya kuweka akiba(fedha) na kukopeshana vinavyoundwa kwa hiari na watu wanaojuana kutoka sehemu moja. Wanakikundi hupata fursa ya kuweka akiba, kupata mikopo na kupata fursa ya huduma ndogondogo za kijamii kama afya na elimu. Mikopo katika vikundi hivi hurudishwa na ziada(riba) nafuu. Mwisho wa mwaka wanachama hugawana hisa, riba na faini zilizokusanywa katika mzunguko kulingana na Idadi ya hisa kila mwanachama alizonunua ndani ya mwaka.
Wadau wa vikundi vya hisa mara nyingi ni watu wa jinsia zote, Wanawake na Wanaume. Kikundi kimoja cha Hisa huwa na wastani wa wanakikundi kati ya 15 mpaka 30. Uzoefu unaonyesha kuwa vikundi vyenye wanachama wengi kupita kiasi huwa vina kosa ufanisi wa Uendeshaji hasa pale kikundi kinapokuwa na tabaka la watu wa kawaida. Ni vizuri kikundi cha hisa kiwe na Idadi ya wanachama wasiozidi thelathini (30).
Faida za vikundi vya Hisa ni pamoja na
v  Kusaidia wanachama kupata mitaji ya kuanzisha na kuendeleza shughuli za kiuchumi.
v  Ziada ya mkopo (riba) ni kidogo hivyo haimuumizi mkopaji.
v  Mwanachama hupata gawio la faida inayopatikana.
v  Ni rahisi kuweka akiba kutokana na kiasi kiwango kidogo ambacho wanakikundi hukubaliana kwa pamoja.
v  Huwezesha wanakikundi kupata fursa na huduma za kijamii kama afya na elimu.
v  Ni rahisi kuendesha kikundi.
v  Wanakikundi hupata fursa ya kuelimika katika kikundi.

Shirika la BUFADESO lina wanachama wanaonufaika na mfumo wa Hisa. Asilimia 60 ya wanachama wa shirika wanapata huduma za Mfumo wa Hisa katika vikundi vyao. BUFADESO hutoa elimu ya uandaaji, uanzishaji, uimarishaji wa vikundi vya Hisa kwa maendeleo ya wakulima, wafugaji na wavuvi wa wilaya ya Bunda.

Hakuna maoni:

Chapisha Maoni

Kauli mbiu yetu

BUFADESO kwa maendeleo ya wakulima

MUHIMU

Makala na picha zinazochapishwa katika blogu hii ni kwa ajili ya taarifa na kumbukumbu za Shirika la Bunda Farmers Development Support Organization (BUFADESO)
Hairuhusiwi kutumia yaliyomo katika blogu hii (HASA PICHA) kwa shughuli zozote bila ruhusa ya mmiliki wa blogu hii ambaye ni BUFADESO