Jumanne, 28 Machi 2017

KABILI FUNZA WAHARIBIFU WA MAHINDI

Katika msimu huu wa kilimo, zao la mahindi katika maneneo mengi limevamiwa na funza waharibifu.
Wakulima wengi wamekata tamaa kutokana na mashambulizi ambayo yana athiri sana zao za mahindi kwa sasa.

Kukabiliana na funza hawa. Jaribu kutumia dawa ya kuuwa wadudu ijulikanayo kama NINJA. Dawa hii inaonyesha matokeo mazuri ya kupambana na funza hawa. Ili kupata matokeo mazuri zaidi inashauriwa kutumia angalau mara mbili. Mara ya pili, nyunyuzia baada ya siku tatu tangu ulipotumia kwa mara ya kwanza.

Jumatano, 22 Machi 2017

LEO NI SIKU YA MAJI DUNIANI

Leo ni siku ya maji duniani. Siku hii imeanzishwa ili kukumbusha na kuadhimisha umuhimu wa maji katika maisha ya mwanadamu na viumbe wote hai waliomo. MAJI NI UHAI. Kauli hii inatokana na umuhimu wa maji katika maisha yetu ya kila siku. Maji yanachukua 71% ya eneo lote duniani.
Dhima ya siku ya maji kwa mwaka huu 2017, inasema "MAJI TAKA" Dhima hii inalenga na kuangaza kuwa katika jamii hakuna maji taka bali bali jamii ndio inachafua maji kwa taka. Lengo la dhima hii ni kuhamasisha jamii kulinda maji dhidi ya taka. Uchafuzi wa maji kwa kuweka taka kunasababisha madhara yanayoathiri ubora wa maji. Hivyo ni jukumu la kila mwanajamii kuhakikisha analinda maji na vyanzo vyake.

KWA NINI TUNASEMA MAJI NI UHAI
1. Usipokunyuwa maji utakufa haraka
Kwa ufupi, ni dhahiri kuwa usipokunywa maji utakufa. Maji ni muhimu zaidi kwenye mwili wa binadamu hata kuliko chakula. Ni dhahiri kwamba sipokula chakula utakufa, lakini utakufa ndani ya siku chache zaidi kama hautakunywa maji.
2. Huzuia Saratani
Tafiti mbalimbali zinaonesha kuwa watu wenye tabia za kunywa maji mengi kadri inavyotakiwa (angalau lita 3 kwa siku) wana nafasi nzuri zaidi ya kupunguza uwezekano wa kupata saratani kwa asilimia 45.
3.  Hupunguza msongo wa mawazo
Tafiti mbalimbali zinaonesha kuwa ukosefu wa maji ya kutosha mwilini kunaweza kuathiri uwezo wa kufikiria wa binadamu na kumfanya aweze kuchanganyikiwa na mambo kwa uharaka zaidi kuliko mtu ambaye anakunywa maji mengi. Mtu anayekunjwa maji mengi huwa na uwezo mzuri wa kufikiria kwa utulivu na kuikaribisha furaha zaidi.Ukiwa na msongo wa mawazo, utakuwa katika wakati mgumu zaidi endapo utakuwa haunywi maji mengi kwa kuwa uwezo wako wa kufikiria umeathiriwa na ukosefu wa maji.
4. Huongeza uwezo wa kufanya kazi
Mwili wa binadamu ni kama mashine inayofanya kazi kwa kutumia mfumo wa umeme hivyo hupata joto au kuchoka na huitaji kutulizwa. Maji ni dawa bora zaidi kwa mwili wa binadamu kwa kuwa husaidia kurekebisha joto la mwili na kuondoa uchovu hivyo kufanya kazi vizuri zaidi.
Mtu anaekunywa maji mengi, huwa na uwezo mkubwa zaidi wa kufanya kazi sio tu zile za kutmia nguvu lakini pia zile ambazo hutumia akili kwa kiwango cha hali juu cha kuuchosha ubongo. Kutokunywa maji kwa kiwango kinachotakiwa hupelekea uchovu wa haraka, usingizi na kuzubaa pamoja na unyonge wa mwili. Kutokunywa maji mengi husababisha maumivu ya kichwa yasiyo ya lazima.
5. Hupunguza Uzito.
Kunywa maji mengi kunapunguza sana uwezekano wa kula vyakula mara kwa mara. Hii ni kwa sababu mara nyingi watu huhisi wana njaa na kulazimika kula ili kuiondoa njaa hiyo hivyo tumbo kujazwa vyakula wakati wote na kupelekea kuwa na uzito/unene uliopitiliza.
Kunywa maji mengi mara kwa mara kunaondoa hali ya kutaka kula mara kwa mara kwa kuwa mwili unakuwa na nguvu hivyo kuupunguza mwili kwa kiasi kinachotakiwa.
6. Huondoa maumivu ya viungo
Watu wengi wanasumbuliwa na tatizo la viungo vya mwili kupata maumivu au kuchoka sana lakini watu hao bahati mbaya hukimbilia tiba za madawa kabla ya kujiuliza kama wana maji ya kutosha mwilini. Kunywa maji mengi husaidi kuondoa maumivu ya viuongo na kuufanya viungo hivyo kuwa na ulaini unaofaa.
7. Huondoa Uchafu na ‘acid’
Kunywa maji mengi husaidia kusafisha kibofu cha mkojo kwa hali inayofaa. Mwili huondoa kiasi kikubwa sana cha uchafu unaotakiwa kutoka mwilini kwa njia ya mkojo na jasho. Mtu anayekunywa maji mengi hujikuta anatoa maji mengi mwilini yanayotoka na uchafu usiofaa mwilini hivyo kuufanya mwili kuwa katia hali nzuri ya kufanya kazi na kuzalisha virutubisho.
Pia maji husaidia mashine za mwili kufanya kazi kwa kiwango kizuri katika kuchuja na kuchakata vyakula kupata virutubisho. Maji mengi husaidia kuondokana na uwezekano wa kuvimbiwa.
8. Husaidia matunzo bora ya ngozi
Ngozi huchukua sehemu kubwa zaidi ya miili yetu hivyo ni eneo ambalo linapaswa kuangaliwa na kupewa matunzo ya hali ya juu. Kunywa maji kwa wingi kunasaidia ubora wa ngozi na kung’arisha rangi ya ngozi husika kwa kiwango kinachotakiwa. Inasaidia pia katika kujenga zaidi seli za mwili.
Hizo ni faida chache za Maji katika mwili wa binadamu ambazo zinakupa sababu zaidi ya kunywa maji mengi kadri iwezekanavyo. Kwa kawaida unashauriwa kutumia angalau lita mbili na nusu hadi tatu za maji kila siku.
Kiasi hicho cha maji kinaweza kuwa kigumu sana kunywa kutokana na maisha ya mihangaiko ya watanzania wengi. Lakini, ili kukamilisha kiwango hicho kwa faida ya mwili wako, unapaswa kuhakikisha kuwa popote ulipo una uko karibu na chupa kubwa ya maji na unaitumia ipasavyo.
Unapaswa kunywa maji mengi hadi pale utakapoanza kukojoa angalau mara kadhaa na mkojo uwe mweupe sana. Mhimize sana rafiki, mpenzi na ndugu yako kuhusu zoezi la kunywa maji.  Na kwa wana familia, hakikisha mnakunywa maji kwa wingi na inakuwa tabia na taratibu za familia.
Ili kunywa maji mengi zaidi, epuka kunywa maji ya baridi sana. Maji yenye uvuguvugu kidogo au yasiyotoka kwenye majokofu yanapendekezwa zaidi na wataalam wa masuala ya afya kama tiba sahihi ya mwili wa binadamu.

Jumanne, 21 Februari 2017

UFUGAJI WA KUKU WA KIENYEJI

Kuku wa kienyeji ni kuku wanaopendwa kufugwa na kuliwa na watu wengi kutokana na uasili wake. Jina la kuku wa kienyeji limekuwa maarufu kutokana na asili(mbegu) ya kuku hawa kutoka katika mazingira yetu tunayoishi, pia mazingira ya ufugaji wake. Ni dhahiri kwa sasa kuku wa kienyeji wamekuwa ghali na wana thamani kubwa kuliko kuku wa kisasa. hii inadhirisha ubora wake na sifa zake kama zinavyoainishwa hapa chini:

A.SIFA ZA KUKU WA KIENYEJI
1. Wanavumilia magonjwa. Kuku wa kienyeji ni wastahimilivu wa magonjwa lakini ni muhimu wakikingwa na magonjwa ya kuku kama mdondo, ndui ya kuku n.k kwa kuwapa chanjo ili kuweza kuwaendeleza.
2. Wana uwezo wa kujitafutia chakula ardhini. Wanao uwezo wa kuchangamka katika mazingira kwa kuparuaparua ili wapate chakula.
3. Wana uwezo wa kuatamia mayai, kutotoa na kulea vifaranga na ustahimilivu wa mazingira magumu kama ukame, baridi n.k
4.Nyama na mayai yake vina ladha nzuri kuliko kuku wa kisasa. Pia virutubisho vilivyomo katika mayai na nyama ya kuku wa kienyeji ni vingi kuliko kuku wa kisasa.
5. Wana uwezo wa kujilinda na maadui kama mwewe n.k . Pamoja na sifa hizi ni muhimu muhimu kuku hao wakapewa matunzo mazuri, wakawekwa kwenye mabanda mazuri, wakapewa maji na chakula cha kutosha.

B.FAIDA ZA KUKU WA KIENYEJI.
-1. Mayai huweza kutumika kwa tiba.  
-2. Kiini cha njano cha yai kinaweza kutumika kutengenezea mafuta ya nywele (shampoo)
-3. Manyoya yake yanaweza kutumika kama mapambo.
-4. Kinyesi cha kuku kinaweza kutumika kama mbolea kwa mazao na pia kama chakula cha samaki.
-5. Nyama ya kuku ni kotoweo kitamu kinachopendwa na kila mtu.
-6. Tangu enzi jogoo amekuwa akitumika kutumbusha muda/wakati hasa wakati wa alfajiri pale anapowika.
-7. Kuku wakifugwa vizuri ni ajira yenye faida kubwa kwa mfugaji.
 

C:MAPUNGUFU
Yako mapungufu mengi yanayofahamika lakini hapa naomba niweke lile la muhimu zaidi. MAGONJWA kama mdondo na ndui huathiri ufugaji wa kuku kutokana na kutokuzingatia kuchanja kuku kwa wakati.


D: KABILA ZA KUKU WA KIENYEJI
Kuna maelezo ya kusisimua sana kuhusu makabila ya kuku wa kienyeji, hata hivyo kuna ugumu kidogo kuweza kuyachanganua makabila hayo kutokana na muingiliano mkubwa wa vizazi kati ya aina mbalimbali za kuku hao. Hata hivyo kuku hawa wana tofauti za kimaumbile zinazosaidia kwa kiasi fulani kutambua uwepo wa baadhi ya makabila ya kuku. Kabila hizi pia zinahusishwa kwa kiasi kikubwa na eneo kuku wanakotoka. Baadhi ya kuku wa kienyeji wanaweza kutambuliwa kwa maumbile yao Mfano:

a.
 Kishingo - kuku wasio na manyoya shingoni
b.
 Njachama au Nungunungu - Hawa ni wale wenye manyoya yaliyosimama.
c.
 Kibwenzi - Ni wale wenye manyoya mengi kichwani.
d.
 Kibutu- Hawa hawana manyoya mkiani
Mwingiliano wa vizazi unaweza ukasababisha kuku kuwa na aina ya maumbile mchanganyiko. Mfano kuku aina ya kuchi anaweza kuwa na alama ya kishingo, Njachama, Kibwenzi au Kibutu.

Hivyo kabila za kuku zifuatazo zinaweza kutambuliwa kama ndiyo kabila za kuku wa kienyeji kulingana na maumbile yao na maeneo wanakotoka.
(i)          KUCHI
Ni kuku warefu kwa umbo na wenye kusimama mgongo ukiwa wima. Wana manyoya machache mwilini na hasa kifuani, vilemba vyao ni vidogo. Majogoo huwa na wastani wa uzito wa Kg. 2.5 na mitetea kg 1.5 mayai ya kuchi yana uzito wa wastani wa gm 45. Kuku hawa hupatikana kwa wingi maeneo ya Mwanza, Shinyanga, Tabora na Zanzibar.

(ii) CHING'WEKWE

Kuku hawa ambao jina lao ni gumu kidogo kwa mtu asiyekuwa na meno kulitamka wana sifa zifuatazo.
Majogoo wana wastani wa kg 1.6, Mitetea wastani kg 1.2, mayai wastani wa gm 37. Kuku hawa wenye umbo dogo hupatikana zaidi maeneo ya CHAKWALE mkoani Morogoro na pia sehemu za umasaini. Kuku hawa hutaga mayai mengi sana kuliko aina nyingine ya kuku wa kienyeji waliopo Tanzania, kwa hiyo wanafaa sana kwa biashara ya mayai.


(iii)UMBO LA KATI

Majogoo wana uzito wa wastani wa kg. 1.9, Mitetea kg. 1.1, Kuku hawa ndio hasa wanaoitwa wa kienyeji(wa kawaida) Wana rangi tofauti. Utafiti umeonyesha kuwa kuku hawa hukua upesi na hupata kinga upesi baada ya kuwachanja dhidi ya ugonjwa wa mdondo (Castle desease)
Muhimu - Mfugaji akifanya uchaguzi kutoka kwenye aina hii ya kuku na kutoa matunzo mazuri kwa hao kuku waliochaguliwa, Hakika anaweza kupata kuku walio bora na wenye uzito wa kutosha pia kutaga mayai mengi na makubwa.


(iv) SINGAMAGAZI

Ni aina ya kuku wakubwa wa kienyeji wanaopatikana zaidi TABORA, kuku hawa wana utambulisho maalum kutokana na rangi zao. Majogoo huwa na rangi ya moto na mitetea huwa na rangi ya nyuki. Uzito - Majogoo uzito wa wastani wa kg 2.9, mitetea wastani wa kilo 2 mayai gramu 56.

(v) MBEYA
Kuku hawa wanapatikana Ileje mkoani mbeya. Asili hasa ya kuku hawa ni kutoka nchi ya jirani ya Malawi na si wa kienyeji asilia bali wana damu ya kuku wa Kizungu "Black Australop". Majogoo Kg 3 mitetea kg 2 mayai gram 49

(vi) PEMBA 
Hupatikana zaidi Pemba. Majogoo Kg.1.5 Mitetea Kg 1 mayai wastani gm 42

(vii) UNGUJA.
Majogoo Kg 1.6, mitetea kg 1.2 mayai gm 42. Kuku hawa wa Unguja na Pemba wanashabihiana sana na Kuchi isipokuwa hawa ni wadogo.
u

KWA UFUGAJI BORA WA KUKU WA KIENYEJI YAPASWA KUZINGATIA YAFUATAYO:
I. Usafi wa vyombo na mazingira ya kuku
Eneo na banda la kufugia kuku wako yapaswa liwekwe safi muda wote kwa kuzingatia yafuatayo:
1.  Vyombo vya chakula na maji visafishwe mara kwa mara kwa maji safi na sabuni.
2.  Pumba au chakula kilicholowana na kuchanganyika na kinyesi cha kuku kitolowe na kufukiwa.
3.  Choma moto au zika kwenye shimo refu kuku waliokufa kwa ugonjwa.
4.  Usifuge kuku na ndege wa jamii nyingine kwa mfano bata katika banda moja.
5.  Ondoa mbolea mara kwa mara kutoka katika banda la kuku.
6.  Tumia dawa za kuulia vimelea kusafishia banda na upake chokaa angalau mara moja kwa mwaka.
7.  Ziba matundu yote yanayoweza kuruhusu panya na wanyama wakali kama vicheche kuingia katika banda la kuku.

II. Wapatie kinga na tiba kuku wako kila mara:
Changamoto kubwa ya ufugaji wa kuku ni kuathiriwa na magonjwa. zingatia na kuwa makini katika kukabiliana na changamoto hii. Magonjwa yanayoshambulia kuku ni pamoja na:
Ndui ya kuku
Huathiri sana vifaranga wanaokua na ujitokeza kwa wingi wakati wa mvua za muda mrefu. Husababisha vivimbe katika uso/ kishungi na hata sehemu nyengine zisizo na manyoya.
Mdondo/kideri
Mdondo, au kwa majina mengine lufuo, au kideri ni ugonjwa hatari katika magonjwa ya kuku wa asili. Ni ugojwa wa virusi ambao huathiri kuku wa rika zote, huweza kuangamiza kuku wote kijijni.
Ukosefu wa vitamini A
Ugonjwa huu husababisha macho kuvimba na kutoa uchafu mziito kama sabuni iliyolowana. Kuku wenye dalili hizi hawaponi na hata kufa. Ugonjwa hujitokeza baada ya kipindi kirefu cha kiangazi kwa ajili ya ukosefu wa majani mabichi.
Kosidiosisi
Huathiri kuku wa umri wowote lakini huuwa zaidi vifaranga na kuku wanaokua. Kuku hudhoofika, manyoya huvurugika na kuku huwa kama wamevaa koti. Kuku huarisha damu au kinyesi cha kahawia na huzubaa na kuonekana kama wamevaa koti.
Viroboto, chawa na utitiri
Hawa ni wadudu wa nje wanaoshambulia ngozi. Huweza kusababisha ugonjwa kutokana na kunyonya damu. Viroboto hushambulia kichwa na kunata huku wakinyonya damu. Viroboto huuwa vifaranga. Chawa na utitiri hughasi kuku hadi wakashindwa kutaga na kuatamia.
Minyoo
Minyoo huweza kudhofisha kuku na kuwafanya waweze kuugua maradhi mengine kirahisi. Muone mtaalaam ukihisi kuku wako wana minyoo.
III. Wape kuku Chakula cha kutosha
1.  Wapatie vifaranga nyongeza ya protini kwa kuwachanganyia vumbi la dagaa au vichwa vya dagaa vilivyotwangwa kwenye pumba za mahindi.
2.  Changanya kikombe kimoja cha vumbi la dagaa na vikombe vitano vya pumba za mahindi (tumia kikombe kidogo cha chai).
3.  Mchwa na wadudu wengine wanaweza kutumika kama nyongeza ya protini.
4.  Vuna mchwa kwenye vichuguu au tengeneza mchwa katika njia za mchwa.
5.  Kutengeneza mchwa: changanya kinyesi cha ng’ombe na majani makavu, mabua ya mahindi au maranda ya mbao katika chungu au ndoo ya zamani.
6.  Mwagia maji hadi kila kilichomo kilowane kisha weka katika chombo kama ndoo au chungu. Weka chombo chako katika njia ya mchwa ukikigeuza juu chini na subiri hadi kesho yake asubuhi, kisha beba vyote vilivyomo na uwamwagie kuku mahali walipo.

IV. Tafuta vifaranga bora
Fanya yafuatayo ili uweze kutotolesha vifaranga bora ambavyo vitakupatia kuku bora na wazuri
Chagua jogoo bora na tetea bora kuzalisha kuku.
Sifa za jogoo bora
1.  Awe na umbo kubwa, awe ukiko mzuri na usioangukia upande mmoja.
2.  Apende kuwa na himaya yake. Ukimpata jogoo mwenye sifa hizi mueke yeye na matetea kumi. Hivyo ukiwa na matetea ishirini jogoo wawili wanatosha.
       Sifa za tetea bora
Tetea bora ni yule mwenye umbo kubwa, mwenye uwezo wa kutaga mayai ya kutosha, kuatamia na hatimaye kutotoa vifaranga.
Uhifadhi wa mayai
1.  Weka mayai mahali safi na penye hewa ya kutosha.
2.  Tumia kasha lililokatwa na kujaza mchanga mkavu na safi au kasha la kuhifadhia mayai.
3.  Weka sehemu butu ya yai iwe upande wa juu na ile iliyochongoka itizame chini.
4.  Andika namba au tarehe katika siku lilipotagwa.
5.  Mayai yakishatagwa yatolewe na kuhifadhiwa na moja liachwe kwenye kiota ili kumuita kuku kuja kutaga kesho yake.
Kuatamiza mayai
1.  Kuku awekewe mayai yatakayokuwa na uwezo wa kuyaatamia na kuyatotoa yote.
2.  Mayi 10 hadi 12 yanatosha kuatamia.
3.  Mayai ya kuatamiza yasizidi wilki 2 toka kutagwa.
4.  Yai la mwisho kutagwa liwe la kwanza kuchaguliwa hadi yapatikane mayai 10 mpaka 12, na apewe kuku wa kuyaatamia.
5.  Mayai ya kuatamiza yasafishwe kwa kitambaa kikavu na safi au kilichowekwa spiriti
Kutotolesha vifaranga wengi kwa wakati mmoja
1.  Kama unataka kuku zaidi ya mmoja watamie na kutotoa kwa mpigo fanya yafuatayo;
2.  Kuku wa kwanza akianza kuatamia muwekee mayai yasiyo na mbegu mfano mayai ya kuku wa kisasa au kuku asiye na jogoo.
3.  Rudia zoezi hilo hadi utakapofikisha kuku watano kisha wawekee kuku wote mayai yenye mbegu.
V. Tunza vizuri vifaranga ili waweze kukua
Vifaranga wengi hufa kabla ya kufikisha miezi miwili kutokana na magonjwa, baridi na kuliwa na wanyama wengine. Ili kupunguza vifo vya vifaranga wa siku 1 hadi miezi miwili zingatia yafuatayo;

Ulinzi dhidi ya mwewe na wanyama wengine
1.  Weka vifaranga kwenye tenga na kuwafunika ili wasiende mbali wakati wa mchana. Wape maji na chakula. Hakikisha hawapigwi jua wala kunyeshewa mvua. Wakati wa usiku walale na mama yao.
Chanjo ya mdondo kideri/lufuo
Kama tetea alichanjwa kabla ya kuanza kutaga vifaranga wanaoanguliwa huwa na kinga ya mdondo ya kuwatosha kwa wiki 3 za kwanza za maisha yao. Wachanje vifaranga hao dhidi ya mdondo wafikishapo umri wa siku 18.
Vifaranga ambao historia ya chanjo ya mama haijulikani, wapewe chanjo ya mdondo siku tatu baada ya kuanguliwa, rudia hadi wakifikisha wiki tatu kisha uchanje kila baada ya miezi 3
Kinga dhidi ya kosidiosisi
Kinga ya kosidiosisi kwa vifaranga, itolewe hata kama ugonjwa haujajitokeza.
1.  Wape dawa ya amprolium kwa muda wa siku tatu mfululizo mara wafikishapo siku saba tokea waanguliwe kama kinga ya kosidiosisi.
2.  Dawa inaweza kutolewa hata kama wamevuka umri huo. Fuata maelekezo ya mtaalam juu ya kiasi cha dawa kinachopaswa kuchanganwa katika maji au pumba
3.  Kama vifaranga wadogo wataonesha dalili za kuzubaa kama kuvaa koti wapewe dawa ya amprolium kwenye maji kwa utaratibu ufuatao;
Dawa siku tatu mfululizo: usiwape kwa siku mbili; gawa tena kwa siku tatu

MAMBO YA JUMLA YA KUZINGATIA
1.  Hakikisha banda na vyombo vya chakula cha kuku ni visafi kuepusha magonjwa.
2.  Usichanganye kuku na bata katika banda moja. 
3.  Lisha chakula cha ziada hasa kwa vifaranga.Unaweza kununua chakula maalum au kujitengenezea mwenyewe.
4.  Kideri, kosidiosisi, ndui na upungufu wa vitamini A ni vyanzo vikuu vya vifo vya kuku wako. Kumbuka kukinga kuku wako dhidi ya magojwa haya.
5.  Kumbuka kuchagua mayai ya kuatamiza kama ilivyoelekezwa ili kuepuka kupata mayai viza.
6.  Vifaranga wadogo hadi wiki nane huhitaji matunzo mazuri, fuata maelezo kuzuia vifo.Kumbuka unapopoteza kifaranga ni hasara kama unavyopoteza kuku mzima tetea/jogoo.
7.  Kumbuka ukiuza kuku wengi kwa mpigo utaongeza mapato yako, jitahidi kuzalisha vifaranga kwa wingi ili upate kuku wengi baadae.
8.  Muone mtaalam wa mifugo ulie karibu nae kwa ushauri zaidi.
9.  Soma maelezo haya mara kwa mara na ufanye yalioelekezwa.
10. Washirikishe wengine katika kaya yako ili nao wajifunze na kufanya hivyo kukuza ufugaji na kipato cha familia.Katika kaya nyingi kuku ni mifugo ya watoto au kinamama. Familia ilishiriki kwa pamoja na kwa usawa, kuku watapata huduma na mahitaji yao na mwisho wa siku faida itanufaisha familia nzima. 

Kauli mbiu yetu

BUFADESO kwa maendeleo ya wakulima

MUHIMU

Makala na picha zinazochapishwa katika blogu hii ni kwa ajili ya taarifa na kumbukumbu za Shirika la Bunda Farmers Development Support Organization (BUFADESO)
Hairuhusiwi kutumia yaliyomo katika blogu hii (HASA PICHA) kwa shughuli zozote bila ruhusa ya mmiliki wa blogu hii ambaye ni BUFADESO