Alhamisi, 7 Juni 2018

MUHTASARI WA HALI YA HEWA KWA MEI, 2018 NA MWELEKEO WA JUNI, 2018


Dondoo za Juni 2018.
Taarifa hii inatoa muhtasari wa hali ya viashiria pamoja na mwenendo wa hali ya hewa kwa mwezi Mei, 2018 na mwelekeo wa viashiria pamoja na hali ya joto kwa mwezi Juni, 2018 nchini.
a) Hali ya joto la chini ya wastani kwa kipindi cha mwezi Juni inatarajiwa hususan katika maeneo ya miinuko.
b) Vipindi vifupi vya upepo mkali vinatarajiwa kujitokeza katika baadhi ya maeneo ya ukanda wote wa pwani wa nchi.
c) Mvua za Masika katika maeneo yanayopata misimu miwili ya mvua zimeisha kati ya wiki ya tatu na ya nne ya mwezi Mei, 2018 kama ilivyotarajiwa.

 MUHTASARI WA HALI YA HEWA KWA KIPINDI CHA MEI, 2018
Katika kipindi cha wiki tatu za mwanzo za mwezi Mei, kulikuwa na mtawanyiko wa kuridhisha wa mvua za Masika katika maeneo yanayopata misimu miwili ya mvua kwa mwaka. Maeneo ya pwani ya kaskazini yalipata mvua nyingi zaidi kwa siku (milimita 70.2 katika kituo cha Pemba na milimita 65.8 kwa kituo cha Zanzibar). Uwepo wa vipindi vya mvua kubwa katika maeneo ya ukanda wa pwani ya kaskazini ulisababisha uharibifu wa barabara hivyo kuathiri usafirishaji, majeruhi na vifo vichache pia viliripotiwa. Maeneo ya nyanda za juu kusini magharibi, magharibi na pwani ya kusini yalipata mvua za nje ya msimu katika kipindi cha mwezi Mei.

MATAZAMIO KWA JUNI, 2018
MIFUMO YA HALI YA HEWA
Hali ya joto la chini ya wastani hadi wastani inatarajiwa kuendelea katika maeneo ya kati ya Kitropiki ya Bahari ya Pasifiki pamoja na pwani ya Somalia, ilihali hali ya joto la juu ya wastani inatarajiwa katika maeneo ya kusini magharibi mwa bahari ya Hindi na pwani ya Angola katika kipindi cha mwezi Juni ,2018. Hali hii ya joto la juu ya wastani katika bahari ya Hindi inatarajiwa kusababisha uwepo wa mvua za nje ya msimu katika ukanda wa pwani. Migandamizo mikubwa ya hewa iliyopo kusini mwa Afrika inatarajiwa kuimarika na hivyo kusababisha hali ya ubaridi katika maeneo mengi hapa nchini na vipindi vya upepo mkali.

HALI YA HEWA KWA KIPINDI CHA MWEZI JUNI, 2018
Katika kipindi cha mwezi Juni, 2018 hali ya joto la wastani hadi chini ya wastani inatarajiwa katika maeneo mengi ya nchi. Hata hivyo vipindi vya baridi vinatarajiwa hususan nyakati za usiku na alfajiri. Ufuatao ni mwelekeo wa hali ya hewa nchini;

Pwani ya kaskazini (Mikoa ya Tanga, Pwani, Dar es Salaam, Morogoro pamoja na visiwa vya Unguja na Pemba): Viwango vya chini vya joto vinatarajiwa kuwa kati ya nyuzi joto 12 hadi 20 katika maeneo mengi. Hata hivyo baadhi ya maeneo ya miinuko ya mkoa wa Tanga hususani wilaya za Lushoto na Bumbuli zinatarajiwa kuwa na kiwango cha chini ya nyuzi joto 12. Hali ya ukavu kwa ujumla pamoja na vipindi kadhaa vya mvua za nje ya msimu inatarajiwa hususan katika kumi la pili la mwezi Juni, 2018.

Nyanda za juu kaskazini mashariki (Mikoa ya Kilimanjaro, Arusha na Manyara): Viwango vya chini vya joto vinatarajiwa kuwa kati ya nyuzi joto 8 hadi 12 katika maeneo mengi. Haya hivyo baadhi ya maeneo ya miinuko yanatarajiwa kuwa na kiwango vya chini ya nyuzi joto 8. Hali ya ukavu kwa ujumla inatarajiwa.

Kanda ya ziwa Victoria (Mikoa ya Kagera, Geita, Shinyanga, Mwanza, Mara na Simiyu): Viwango vya chini vya joto vinatarajiwa kuwa kati ya nyuzi joto 8 hadi 15 katika maeneo mengi. Haya hivyo maeneo ya miinuko ya mikoa ya Kagera na Geita yanatarajiwa kuwa na kiwango vya chini ya nyuzi
joto 8. Hali ya ukavu kwa ujumla inatarajiwa.

Magharibi mwa nchi (Mikoa ya Kigoma, Katavi na Tabora): Viwango vya chini vya joto vinatarajiwa kuwa kati ya nyuzi joto 10 hadi 14 katika maeneo mengi. Hali ya ukavu inatarajiwa.
Kanda ya kati (Mikoa ya Dodoma na Singida): Viwango vya chini vya joto vinatarajiwa kuwa kati ya nyuzi joto 8 hadi 14 katika maeneo mengi. Hali ya ukavu inatarajiwa.

Nyanda za juu kusini magharibi (Mikoa ya Rukwa, Njombe, Iringa na Mbeya): Viwango vya chini vya joto vinatarajiwa kuwa kati ya nyuzi joto 4 hadi 12 katika maeneo mengi. Hata hivyo maeneo ya miinuko pamoja na mkoa wa Njombe yanatarajiwa kuwa na kiwango cha chini ya nyuzi joto 4.
Maeneo ya kusini mwa mkoa wa Morogoro yanatarajiwa kuwa na kiwango cha chini cha joto cha juu ya nyuzi joto 12. Hali ya ukavu inatarajiwa kuendelea katika maeneo mengi, ingawa kuna uwezekano wa vipindi vichache vya mvua hususan katika maeneo ya miinuko (Tukuyu na Njombe).

Pwani ya kusini (Mikoa ya Mtwara na Lindi): Viwango vya chini vya joto vinatarajiwa kuwa kati ya nyuzi joto 12 hadi 18 katika maeneo mengi. Hali ya ukavu inatarajiwa kuendelea.

Kanda ya kusini (Mkoa wa Ruvuma): Viwango vya chini vya joto vinatarajiwa kuwa kati ya nyuzi joto 8 hadi 14 katika maeneo mengi. Maeneo ya miinuko ya mkoa wa Ruvuma yanatarajia kupata chini ya nyuzi joto 8 katika kipindi cha mwezi Juni, 2018.Hali ya ukavu inatarajiwa kuendelea.

Imetolewa na;
MAMLAKA YA HALI YA HEWA TANZANIA

Hakuna maoni:

Chapisha Maoni

Kauli mbiu yetu

BUFADESO kwa maendeleo ya wakulima

MUHIMU

Makala na picha zinazochapishwa katika blogu hii ni kwa ajili ya taarifa na kumbukumbu za Shirika la Bunda Farmers Development Support Organization (BUFADESO)
Hairuhusiwi kutumia yaliyomo katika blogu hii (HASA PICHA) kwa shughuli zozote bila ruhusa ya mmiliki wa blogu hii ambaye ni BUFADESO