JAMHURI YA MUUNGANO WA TANZANIA
WIZARA YA UJENZI, UCHUKUZI NA MAWASILIANO
MAMLAKA YA HALI YA HEWA TANZANIA
MWELEKEO WA MVUA TANZANIA
KIPINDI CHA MSIMU WA MVUA ZA ‘VULI’ OKTOBA – DISEMBA, 2018
DONDOO MUHIMU ZA MSIMU WA VULI OKTOBA HADI DISEMBA, 2018
Taarifa hii inatoa uchambuzi wa mwenendo wa mifumo ya hali ya hewa na mwelekeo wa msimu wa mvua katika kipindi cha Oktoba hadi Disemba, 2018, ushauri na tahadhari kwa wadau wa sekta mbali mbali wanaohitaji taarifa za hali ya hewa katika utekelezaji wa majukumu yao kama vile Kilimo na Usalama wa Chakula, Mifugo na Wanyamapori, Maliasili na Utalii, Uchukuzi na Mawasiliano, Nishati na Maji, Mamlaka za Miji, Afya pamoja na Menejimenti za Maafa. Muhtasari wa mwelekeo wa mvua hizo na athari zake ni kama ifuatavyo:
a) Katika msimu wa mvua za Vuli 2018
Kunatarajiwa kuwa na mvua za wastani katika maeneo mengi pamoja na uwezekano mkubwa wa kupata mvua za juu ya wastani hususan katika maeneo ya Mikoa ya Tanga, Dar es Salaam, Pwani, Morogoro pamoja na visiwa vya Unguja and Pemba.
Ongezeko la mvua linatarajiwa hususan katika mwezi Novemba, 2018 kutokana na uwezekano wa kutokea vimbunga katika eneo la kusini magharibi mwa bahari ya Hindi.
b) Athari
Hali ya unyevunyevu wa udongo katika maeneo mengi yanayotarajiwa kuwa na mvua za wastani na juu ya wastani itatosheleza shughuli za kawaida za kilimo katika maeneo mengi ya mikoa ya Kagera, Mara, Mwanza, Geita, Simiyu, Shinyanga, Kilimanjaro, Arusha, Manyara, Dar es Salaam, Tanga, Pwani ; Visiwa vya Unguja na Pemba pamoja na maeneo ya kusini mwa mkoa wa Morogoro.
Vipindi vifupi vya mvua kubwa vinatarajiwa kujitokeza na hivyo kuongeza uwezekano wa mafuriko hata katika maeneo yanayotarajiwa kupata mvua za wastani hadi chini ya wastani.
I. MWELEKEO WA MSIMU WA MVUA KIPINDI CHA OKTOBA – DISEMBA 2018.
Mifumo ya hali ya hewa inayotarajiwa (Tazama kipengele II cha taarifa hii), inaonesha uwezekano mkubwa wa mvua za vuli kuwa za wastani katika maeneo mengi ya nchi. Aidha, mvua za juu ya wastani zinatarajiwa katika maeneo ya pwani ya kaskazini katika kipindi cha msimu wa mvua wa Oktoba hadi Disemba, 2018. Maelezo ya kina juu ya mwelekeo wa mvua hizo ni kama ifuatavyo:
(i) Mvua za msimu wa Vuli
Mvua za kipindi cha mwezi Oktoba hadi Disemba (Vuli) ni mahususi kwa maeneo yanayopata misimu miwili ya mvua kwa mwaka (Ukanda wa Ziwa Viktoria, nyanda za juu kaskazini mashariki, Ukanda wa Pwani ya kaskazini na wilaya ya Kibondo). Mvua za Vuli 2018 zinatarajiwa kuanza mapema katikati ya mwezi Septemba na mwanzoni mwa Oktoba, 2018 katika maeneo mengi yanayopata misimu miwili ya mvua. Mvua hizo zinatarajiwa kuwa za wastani hadi chini ya wastani katika maeneo ya mkoa wa Kagera, Geita na wilaya ya Kibondo; mvua za wastani hadi juu ya wastani zinatarajiwa katika maeneo ya nyanda za juu kaskazini mashariki pamoja na maeneo ya mashariki na kusini mwa Ziwa Viktoria. Mvua za juu ya wastani zinatarajiwa katika maeneo mengi ya pwani ya kaskazini.
Kanda ya Ziwa Victoria: (Mikoa ya Kagera, Mara, Mwanza, Geita, Simiyu na Shinyanga):
Mvua zinatarajiwa kuanza mapema, kati ya wiki ya pili na ya tatu ya mwezi Septemba, 2018 katika maeneo ya mkoa wa Mara na kusambaa katika mikoa ya Shinyanga, Simiyu, Mwanza, Geita na Kagera ifikapo wiki ya tatu ya mwezi Oktoba, 2018. Mvua zinatarajiwa kuwa za wastani hadi juu ya wastani katika mikoa ya Mwanza, Mara, Shinyanga na Simiyu. Mvua za wastani na vipindi vya mvua za chini ya wastani zinatarajiwa katika mikoa ya Kagera, Geita na wilaya ya Kibondo. Mvua za msimu wa Vuli zinatarajiwa kuisha wiki ya nne ya mwezi
Disemba, 2018 katika maeneo ya mikoa ya Mara na Simiyu, na kwa maeneo mengine ya ukanda wa Ziwa Viktoria mvua zinatarajiwa kuisha kati ya wiki ya kwanza na ya pili ya mwezi Januari, 2019.
Ukanda wa Pwani ya Kaskazini: (Mikoa ya Dar es Salaam, Tanga na Pwani, Visiwa vya Unguja na Pemba pamoja na maeneo ya kaskazini mwa mkoa wa Morogoro):
Mvua zinatarajiwa kuanza mapema wiki ya nne ya mwezi Septemba, 2018. Mvua za juu ya wastani hadi wastani zinatarajiwa katika maeneo mengi. Vipindi vya ongezeko la mvua vinatarajiwa hususan katika ya miezi ya Oktoba na Novemba, 2018. Mvua za Vuli zinatarajiwa kuisha wiki ya tatu ya mwezi Disemba, 2018.
Nyanda za juu Kaskazini Mashariki: (Mikoa ya Kilimanjaro, Arusha na Manyara):
Mvua zinatarajiwa kuanza kati ya wiki ya pili ya mwezi Oktoba, 2018 na zinatarajiwa kuwa za wastani hadi juu ya wastani katika maeneo mengi. Mvua hizi zinatarajiwa kuisha wiki ya pili ya mwezi Disemba, 2018.
Matukio mengi ya mvua kubwa yanatarajiwa kujitokeza hususan katika maeneo yanayotarajiwa kupata mvua za juu ya wastani. Hata hivyo, izingatiwe kuwa matukio ya vipindi vifupi vya mvua kubwa yanatarajiwa hata katika maeneo yanayopata mvua za wastani na chini ya wastani.
II. MIFUMO YA HALI YA HEWA
Hali ya joto la juu ya wastani katika eneo la kati la Kiikweta katika Bahari ya Pasifiki inatarajiwa kuendelea katika kipindi cha Oktoba-Disemba, 2018. Eneo la magharibi mwa bahari ya Hindi linatarajiwa kuwa na joto la juu ya wastani. Hali hiyo sambamba na joto la wastani linalotarajiwa kujitokeza mashariki mwa bahari ya hindi katika miezi ya Oktoba na Novemba itachangia katika uwepo wa upepo wenye unyevunyevu kutoka mashariki kuelekea katika Pwani ya nchi. Aidha, matukio ya Vimbunga yanayotarajiwa kujitokeza katika eneo la kusini magharibi mwa bahari ya Hindi sambamba na hali ya joto la chini ya wastani katika eneo la pwani ya Angola, vinatarajiwa kuchochea msukumo wa upepo wenye unyevunyevu kutoka misitu ya Congo katika maeneo mengi. Hali hivyo inatarajiwa kuchangia vipindi vya kuongezaka kwa mvua hapa nchini. Hata hivyo, hali ya joto la wastani katika eneo la mashariki mwa bahari ya Hindi inatarajiwa kujitokeza mwishoni mwa msimu na kupunguza msukumo chanya kutoka eneo la Kiikweta la bahari ya Pasifiki kwa mwenendo wa mvua katika pwani ya Afrika mashariki.
III. ATHARI NA USHAURI.
Kilimo, Mifugo, Uvuvi na Wanyamapori.
Katika kipindi cha msimu wa mvua za vuli (Oktoba hadi Disemba) 2018 hali ya unyevunyevu wa udongo na upatikanaji wa chakula cha samaki vinatarajiwa kuimarika katika maeneo mengi ya ukanda wa nyanda za juu kaskazini mashariki pamoja na pwani ya kaskazini. Hata hivyo, mazao yasiyohitaji maji mengi yanaweza kuathiriwa na hali ya unyevunyevu wa kupitiliza na maji kutuama. Magonjwa ya wanyama na upotevu wa samaki kutokana na uharibifu wa miundombinu ya kufugia samaki vinaweza kujitokeza kutokana na mvua za juu ya wastani zinazotarajiwa katika maeneo hayo.
Upungufu wa unyevunyevu unaweza kujitokeza katika maeneo yanayotarajiwa kupata mvua za wastani hadi chini ya wastani. Hivyo, wakulima katika maeneo hayo wanashauriwa kupanda mazao yanayotumia muda mfupi kukomaa na yanayostahimili ukame.
Malisho na upatikanaji wa maji kwa ajili ya mifugo na wanyama pori vinatarajiwa kuwa vya kuridhisha katika maeneo mengi yanayotarajiwa kupata mvua za juu ya wastani na wastani. Hata hivyo upungufu wa maji kwa ajili ya mifugo na wanyamapori, ufugaji samaki, kupungua kwa samaki katika maji ya asili kutokana na kupungua kwa chakula cha samaki unaweza kujitokeza katika maeneo machache ya magharibi mwa Ziwa Viktoria. Teknolojia ya uvunaji maji ya mvua iimarishwe ili kukidhi mahitaji ya maji katika kipindi cha ukavu. Pamoja na ushauri huu watumiaji wa taarifa za hali ya hewa wanashauriwa kupata ushauri zaidi kutoka kwa wataalam wa sekta husika ikiwemo maafisa ugani.
Nishati, Madini na Maji
Maeneo yanayotarajiwa kupata mvua za juu ya wastani, yanatarajiwa kuwa na ongezeko la maji katika mabwawa. Wachimbaji madini katika migodi midogomidogo wanashauriwa kuwa makini kwani ongezeko la maji katika udongo linaweza kusababisha mmomonyoko wa ardhi. Wadau katika sekta husika wanashauriwa kuchukua hatua stahiki zikiwemo za kupunguza hasara kwa kuimarisha migodi. Hata hivyo, maeneo yanayotarajiwa kupata mvua za wastani hadi chini ya wastani kina cha maji katika maziwa na mabwawa kinatarajiwa kupungua, hivyo matumizi sahihi ya maji yanapaswa kuzingatiwa.
Mamlaka za miji
Vipindi vifupi vya mvua kubwa vinatarajiwa katika msimu wa mvua, hivyo Mamlaka za Miji pamoja na wananchi kwa ujumla wanashauriwa kuchukua hatua za kuhakikisha mifumo na njia za kupitisha maji zinafanyakazi ili kuepusha maji kutuama na kupelekea mafuriko na uharibifu wa miundombinu pamoja na upotevu wa maisha na mali.
Hatua hizo zinashauriwa kuchukuliwa pia katika maeneo yanayotegemewa kupata mvua za wastani hadi chini ya wastani kutokana na kuwa na uwezekano wa vipindi vifupi vya mvua kubwa.
Afya
Kutokana na uhaba wa maji salama unaotarajiwa kwa shughuli za binadamu ikiwemo usafi hususan katika maeneo yanayotarajiwa kupata mvua za chini ya wastani, milipuko ya magonjwa inaweza kujitokeza. Aidha, maeneo yanayotarajiwa kupata mvua za juu ya wastani pia yana uwezekano wa kukumbwa na milipuko ya magonjwa, hivyo sekta ya Afya inashauriwa kuchukua hatua stahiki kama kugawa dawa za kutibu maji ya kunywa, kuzuia na kuharibu mazalia ya mbu, kudumisha usafi wa mazingira pamoja na hatua nyingine stahiki ili kupunguza athari zinazoweza kujitokeza.
Menejimenti ya Maafa:
Menejimenti za maafa zinashauriwa kuandaa mkakati wa kupunguza athari zinazoweza kujitokeza katika msimu wa mvua za Vuli, 2018. Kuandaa mbinu za kukabiliana na mafuriko na majanga yatokanayo na mafuriko kama vile kuimarisha na kuweka rasilimali tayari kwa ajili ya kukabiliana na maafa, kuandaa vikosi kazi na kamati za maafa na kuandaa maeneo ya kuhudumia waathirika wa mafuriko.
Aidha, inashauriwa kuimarisha njia za mawasiliano katika ngazi mbalimbali ili kuhakikisha taarifa za tahadhari zinaifikia jamii kwa wakati ili kupunguza athari zinazoweza kujitokeza.
Vyombo vya habari:
Vyombo vya habari vinashauriwa kufuatilia, kupata na kusambaza taarifa sahihi za mienendo ya hali ya hewa kutoka Mamlaka ya Hali ya Hewa Tanzania (TMA) na kutumia wataalam wa sekta husika katika kuandaa na kufikisha taarifa za masuala mtambuka ya hali ya hewa kwa jamii. Vile vile vyombo vya habari vinashauriwa kutafuta na kutumia ushauri wa kisekta kutoka kwa watoa taarifa wa sekta mbalimbali zinazotumia taarifa za hali ya hewa ili kuujulisha umma athari za kisekta.
Zingatio: Mwelekeo wa mvua uliotolewa hapa umezingatia zaidi kipindi cha msimu (miezi mitatu) na hali ya mvua katika maeneo makubwa. Hivyo, viashiria vinavyochangia mwenendo wa mifumo ya hali ya hewa na mabadiliko ya muda mfupi katika maeneo madogo utazingatiwa katika uchambuzi wa utabiri wa muda wa kati na mfupi. Watumiaji wa taarifa za utabiri huu wanashauriwa pia kufuatilia tabiri za saa 24, siku 10 pamoja na za mwezi kama zinavyotolewa na Mamlaka ya hali ya Hewa Tanzania.
Mamlaka ya Hali ya Hewa Tanzania itaendelea kufuatilia mwenendo wa mifumo ya hali ya hewa na kutoa taarifa za mwelekeo wa mvua nchini ipasavyo.
Imetolewa na Mamlaka ya Hali ya Hewa Tanzania:
Hakuna maoni:
Chapisha Maoni