Jumapili, 9 Septemba 2018

MWELEKEO WA MVUA TANZANIA

JAMHURI YA MUUNGANO WA TANZANIA
WIZARA YA UJENZI, UCHUKUZI NA MAWASILIANO
MAMLAKA YA HALI YA HEWA TANZANIA
MWELEKEO WA MVUA TANZANIA
KIPINDI CHA MSIMU WA MVUA ZA ‘VULI’ OKTOBA – DISEMBA, 2018

DONDOO MUHIMU ZA MSIMU WA VULI OKTOBA HADI DISEMBA, 2018
Taarifa hii inatoa uchambuzi wa mwenendo wa mifumo ya hali ya hewa na mwelekeo wa msimu wa mvua katika kipindi cha Oktoba hadi Disemba, 2018, ushauri na tahadhari kwa wadau wa sekta mbali mbali wanaohitaji taarifa za hali ya hewa katika utekelezaji wa majukumu yao kama vile Kilimo na Usalama wa Chakula, Mifugo na Wanyamapori, Maliasili na Utalii, Uchukuzi na Mawasiliano, Nishati na Maji, Mamlaka za Miji, Afya pamoja na Menejimenti za Maafa. Muhtasari wa mwelekeo wa mvua hizo na athari zake ni kama ifuatavyo:

a) Katika msimu wa mvua za Vuli 2018
 Kunatarajiwa kuwa na mvua za wastani katika maeneo mengi pamoja na uwezekano mkubwa wa kupata mvua za juu ya wastani hususan katika maeneo ya Mikoa ya Tanga, Dar es Salaam, Pwani, Morogoro pamoja na visiwa vya Unguja and Pemba.
 Ongezeko la mvua linatarajiwa hususan katika mwezi Novemba, 2018 kutokana na uwezekano wa kutokea vimbunga katika eneo la kusini magharibi mwa bahari ya Hindi.

b) Athari
 Hali ya unyevunyevu wa udongo katika maeneo mengi yanayotarajiwa kuwa na mvua za wastani na juu ya wastani itatosheleza shughuli za kawaida za kilimo katika maeneo mengi ya mikoa ya Kagera, Mara, Mwanza, Geita, Simiyu, Shinyanga, Kilimanjaro, Arusha, Manyara, Dar es Salaam, Tanga, Pwani ; Visiwa vya Unguja na Pemba pamoja na maeneo ya kusini mwa mkoa wa Morogoro.
 Vipindi vifupi vya mvua kubwa vinatarajiwa kujitokeza na hivyo kuongeza uwezekano wa mafuriko hata katika maeneo yanayotarajiwa kupata mvua za wastani hadi chini ya wastani.

I. MWELEKEO WA MSIMU WA MVUA KIPINDI CHA OKTOBA – DISEMBA 2018.
Mifumo ya hali ya hewa inayotarajiwa (Tazama kipengele II cha taarifa hii), inaonesha uwezekano mkubwa wa mvua za vuli kuwa za wastani katika maeneo mengi ya nchi. Aidha, mvua za juu ya wastani zinatarajiwa katika maeneo ya pwani ya kaskazini katika kipindi cha msimu wa mvua wa Oktoba hadi Disemba, 2018. Maelezo ya kina juu ya mwelekeo wa mvua hizo ni kama ifuatavyo:

(i) Mvua za msimu wa Vuli

Mvua za kipindi cha mwezi Oktoba hadi Disemba (Vuli) ni mahususi kwa maeneo yanayopata misimu miwili ya mvua kwa mwaka (Ukanda wa Ziwa Viktoria, nyanda za juu kaskazini mashariki, Ukanda wa Pwani ya kaskazini na wilaya ya Kibondo). Mvua za Vuli 2018 zinatarajiwa kuanza mapema katikati ya mwezi Septemba na mwanzoni mwa Oktoba, 2018 katika maeneo mengi yanayopata misimu miwili ya mvua. Mvua hizo zinatarajiwa kuwa za wastani hadi chini ya wastani katika maeneo ya mkoa wa Kagera, Geita na wilaya ya Kibondo; mvua za wastani hadi juu ya wastani zinatarajiwa katika maeneo ya nyanda za juu kaskazini mashariki pamoja na maeneo ya mashariki na kusini mwa Ziwa Viktoria. Mvua za juu ya wastani zinatarajiwa katika maeneo mengi ya pwani ya kaskazini.

Kanda ya Ziwa Victoria: (Mikoa ya Kagera, Mara, Mwanza, Geita, Simiyu na Shinyanga):
Mvua zinatarajiwa kuanza mapema, kati ya wiki ya pili na ya tatu ya mwezi Septemba, 2018 katika maeneo ya mkoa wa Mara na kusambaa katika mikoa ya Shinyanga, Simiyu, Mwanza, Geita na Kagera ifikapo wiki ya tatu ya mwezi Oktoba, 2018. Mvua zinatarajiwa kuwa za wastani hadi juu ya wastani katika mikoa ya Mwanza, Mara, Shinyanga na Simiyu. Mvua za wastani na vipindi vya mvua za chini ya wastani zinatarajiwa katika mikoa ya Kagera, Geita na wilaya ya Kibondo. Mvua za msimu wa Vuli zinatarajiwa kuisha wiki ya nne ya mwezi

Disemba, 2018 katika maeneo ya mikoa ya Mara na Simiyu, na kwa maeneo mengine ya ukanda wa Ziwa Viktoria mvua zinatarajiwa kuisha kati ya wiki ya kwanza na ya pili ya mwezi Januari, 2019.
Ukanda wa Pwani ya Kaskazini: (Mikoa ya Dar es Salaam, Tanga na Pwani, Visiwa vya Unguja na Pemba pamoja na maeneo ya kaskazini mwa mkoa wa Morogoro):
Mvua zinatarajiwa kuanza mapema wiki ya nne ya mwezi Septemba, 2018. Mvua za juu ya wastani hadi wastani zinatarajiwa katika maeneo mengi. Vipindi vya ongezeko la mvua vinatarajiwa hususan katika ya miezi ya Oktoba na Novemba, 2018. Mvua za Vuli zinatarajiwa kuisha wiki ya tatu ya mwezi Disemba, 2018.

Nyanda za juu Kaskazini Mashariki: (Mikoa ya Kilimanjaro, Arusha na Manyara):
Mvua zinatarajiwa kuanza kati ya wiki ya pili ya mwezi Oktoba, 2018 na zinatarajiwa kuwa za wastani hadi juu ya wastani katika maeneo mengi. Mvua hizi zinatarajiwa kuisha wiki ya pili ya mwezi Disemba, 2018.

Matukio mengi ya mvua kubwa yanatarajiwa kujitokeza hususan katika maeneo yanayotarajiwa kupata mvua za juu ya wastani. Hata hivyo, izingatiwe kuwa matukio ya vipindi vifupi vya mvua kubwa yanatarajiwa hata katika maeneo yanayopata mvua za wastani na chini ya wastani.

II. MIFUMO YA HALI YA HEWA
Hali ya joto la juu ya wastani katika eneo la kati la Kiikweta katika Bahari ya Pasifiki inatarajiwa kuendelea katika kipindi cha Oktoba-Disemba, 2018. Eneo la magharibi mwa bahari ya Hindi linatarajiwa kuwa na joto la juu ya wastani. Hali hiyo sambamba na joto la wastani linalotarajiwa kujitokeza mashariki mwa bahari ya hindi katika miezi ya Oktoba na Novemba itachangia katika uwepo wa upepo wenye unyevunyevu kutoka mashariki kuelekea katika Pwani ya nchi. Aidha, matukio ya Vimbunga yanayotarajiwa kujitokeza katika eneo la kusini magharibi mwa bahari ya Hindi sambamba na hali ya joto la chini ya wastani katika eneo la pwani ya Angola, vinatarajiwa kuchochea msukumo wa upepo wenye unyevunyevu kutoka misitu ya Congo katika maeneo mengi. Hali hivyo inatarajiwa kuchangia vipindi vya kuongezaka kwa mvua hapa nchini. Hata hivyo, hali ya joto la wastani katika eneo la mashariki mwa bahari ya Hindi inatarajiwa kujitokeza mwishoni mwa msimu na kupunguza msukumo chanya kutoka eneo la Kiikweta la bahari ya Pasifiki kwa mwenendo wa mvua katika pwani ya Afrika mashariki.

III. ATHARI NA USHAURI.
Kilimo, Mifugo, Uvuvi na Wanyamapori.
Katika kipindi cha msimu wa mvua za vuli (Oktoba hadi Disemba) 2018 hali ya unyevunyevu wa udongo na upatikanaji wa chakula cha samaki vinatarajiwa kuimarika katika maeneo mengi ya ukanda wa nyanda za juu kaskazini mashariki pamoja na pwani ya kaskazini. Hata hivyo, mazao yasiyohitaji maji mengi yanaweza kuathiriwa na hali ya unyevunyevu wa kupitiliza na maji kutuama. Magonjwa ya wanyama na upotevu wa samaki kutokana na uharibifu wa miundombinu ya kufugia samaki vinaweza kujitokeza kutokana na mvua za juu ya wastani zinazotarajiwa katika maeneo hayo.
Upungufu wa unyevunyevu unaweza kujitokeza katika maeneo yanayotarajiwa kupata mvua za wastani hadi chini ya wastani. Hivyo, wakulima katika maeneo hayo wanashauriwa kupanda mazao yanayotumia muda mfupi kukomaa na yanayostahimili ukame.

Malisho na upatikanaji wa maji kwa ajili ya mifugo na wanyama pori vinatarajiwa kuwa vya kuridhisha katika maeneo mengi yanayotarajiwa kupata mvua za juu ya wastani na wastani. Hata hivyo upungufu wa maji kwa ajili ya mifugo na wanyamapori, ufugaji samaki, kupungua kwa samaki katika maji ya asili kutokana na kupungua kwa chakula cha samaki unaweza kujitokeza katika maeneo machache ya magharibi mwa Ziwa Viktoria. Teknolojia ya uvunaji maji ya mvua iimarishwe ili kukidhi mahitaji ya maji katika kipindi cha ukavu. Pamoja na ushauri huu watumiaji wa taarifa za hali ya hewa wanashauriwa kupata ushauri zaidi kutoka kwa wataalam wa sekta husika ikiwemo maafisa ugani.

Nishati, Madini na Maji
Maeneo yanayotarajiwa kupata mvua za juu ya wastani, yanatarajiwa kuwa na ongezeko la maji katika mabwawa. Wachimbaji madini katika migodi midogomidogo wanashauriwa kuwa makini kwani ongezeko la maji katika udongo linaweza kusababisha mmomonyoko wa ardhi. Wadau katika sekta husika wanashauriwa kuchukua hatua stahiki zikiwemo za kupunguza hasara kwa kuimarisha migodi. Hata hivyo, maeneo yanayotarajiwa kupata mvua za wastani hadi chini ya wastani kina cha maji katika maziwa na mabwawa kinatarajiwa kupungua, hivyo matumizi sahihi ya maji yanapaswa kuzingatiwa.

Mamlaka za miji
Vipindi vifupi vya mvua kubwa vinatarajiwa katika msimu wa mvua, hivyo Mamlaka za Miji pamoja na wananchi kwa ujumla wanashauriwa kuchukua hatua za kuhakikisha mifumo na njia za kupitisha maji zinafanyakazi ili kuepusha maji kutuama na kupelekea mafuriko na uharibifu wa miundombinu pamoja na upotevu wa maisha na mali.
Hatua hizo zinashauriwa kuchukuliwa pia katika maeneo yanayotegemewa kupata mvua za wastani hadi chini ya wastani kutokana na kuwa na uwezekano wa vipindi vifupi vya mvua kubwa.

Afya
Kutokana na uhaba wa maji salama unaotarajiwa kwa shughuli za binadamu ikiwemo usafi hususan katika maeneo yanayotarajiwa kupata mvua za chini ya wastani, milipuko ya magonjwa inaweza kujitokeza. Aidha, maeneo yanayotarajiwa kupata mvua za juu ya wastani pia yana uwezekano wa kukumbwa na milipuko ya magonjwa, hivyo sekta ya Afya inashauriwa kuchukua hatua stahiki kama kugawa dawa za kutibu maji ya kunywa, kuzuia na kuharibu mazalia ya mbu, kudumisha usafi wa mazingira pamoja na hatua nyingine stahiki ili kupunguza athari zinazoweza kujitokeza.

Menejimenti ya Maafa:
Menejimenti za maafa zinashauriwa kuandaa mkakati wa kupunguza athari zinazoweza kujitokeza katika msimu wa mvua za Vuli, 2018. Kuandaa mbinu za kukabiliana na mafuriko na majanga yatokanayo na mafuriko kama vile kuimarisha na kuweka rasilimali tayari kwa ajili ya kukabiliana na maafa, kuandaa vikosi kazi na kamati za maafa na kuandaa maeneo ya kuhudumia waathirika wa mafuriko.
Aidha, inashauriwa kuimarisha njia za mawasiliano katika ngazi mbalimbali ili kuhakikisha taarifa za tahadhari zinaifikia jamii kwa wakati ili kupunguza athari zinazoweza kujitokeza.

Vyombo vya habari:
Vyombo vya habari vinashauriwa kufuatilia, kupata na kusambaza taarifa sahihi za mienendo ya hali ya hewa kutoka Mamlaka ya Hali ya Hewa Tanzania (TMA) na kutumia wataalam wa sekta husika katika kuandaa na kufikisha taarifa za masuala mtambuka ya hali ya hewa kwa jamii. Vile vile vyombo vya habari vinashauriwa kutafuta na kutumia ushauri wa kisekta kutoka kwa watoa taarifa wa sekta mbalimbali zinazotumia taarifa za hali ya hewa ili kuujulisha umma athari za kisekta.
Zingatio: Mwelekeo wa mvua uliotolewa hapa umezingatia zaidi kipindi cha msimu (miezi mitatu) na hali ya mvua katika maeneo makubwa. Hivyo, viashiria vinavyochangia mwenendo wa mifumo ya hali ya hewa na mabadiliko ya muda mfupi katika maeneo madogo utazingatiwa katika uchambuzi wa utabiri wa muda wa kati na mfupi. Watumiaji wa taarifa za utabiri huu wanashauriwa pia kufuatilia tabiri za saa 24, siku 10 pamoja na za mwezi kama zinavyotolewa na Mamlaka ya hali ya Hewa Tanzania.
Mamlaka ya Hali ya Hewa Tanzania itaendelea kufuatilia mwenendo wa mifumo ya hali ya hewa na kutoa taarifa za mwelekeo wa mvua nchini ipasavyo.

Imetolewa na Mamlaka ya Hali ya Hewa Tanzania:

Alhamisi, 7 Juni 2018

MUHTASARI WA HALI YA HEWA KWA MEI, 2018 NA MWELEKEO WA JUNI, 2018


Dondoo za Juni 2018.
Taarifa hii inatoa muhtasari wa hali ya viashiria pamoja na mwenendo wa hali ya hewa kwa mwezi Mei, 2018 na mwelekeo wa viashiria pamoja na hali ya joto kwa mwezi Juni, 2018 nchini.
a) Hali ya joto la chini ya wastani kwa kipindi cha mwezi Juni inatarajiwa hususan katika maeneo ya miinuko.
b) Vipindi vifupi vya upepo mkali vinatarajiwa kujitokeza katika baadhi ya maeneo ya ukanda wote wa pwani wa nchi.
c) Mvua za Masika katika maeneo yanayopata misimu miwili ya mvua zimeisha kati ya wiki ya tatu na ya nne ya mwezi Mei, 2018 kama ilivyotarajiwa.

 MUHTASARI WA HALI YA HEWA KWA KIPINDI CHA MEI, 2018
Katika kipindi cha wiki tatu za mwanzo za mwezi Mei, kulikuwa na mtawanyiko wa kuridhisha wa mvua za Masika katika maeneo yanayopata misimu miwili ya mvua kwa mwaka. Maeneo ya pwani ya kaskazini yalipata mvua nyingi zaidi kwa siku (milimita 70.2 katika kituo cha Pemba na milimita 65.8 kwa kituo cha Zanzibar). Uwepo wa vipindi vya mvua kubwa katika maeneo ya ukanda wa pwani ya kaskazini ulisababisha uharibifu wa barabara hivyo kuathiri usafirishaji, majeruhi na vifo vichache pia viliripotiwa. Maeneo ya nyanda za juu kusini magharibi, magharibi na pwani ya kusini yalipata mvua za nje ya msimu katika kipindi cha mwezi Mei.

MATAZAMIO KWA JUNI, 2018
MIFUMO YA HALI YA HEWA
Hali ya joto la chini ya wastani hadi wastani inatarajiwa kuendelea katika maeneo ya kati ya Kitropiki ya Bahari ya Pasifiki pamoja na pwani ya Somalia, ilihali hali ya joto la juu ya wastani inatarajiwa katika maeneo ya kusini magharibi mwa bahari ya Hindi na pwani ya Angola katika kipindi cha mwezi Juni ,2018. Hali hii ya joto la juu ya wastani katika bahari ya Hindi inatarajiwa kusababisha uwepo wa mvua za nje ya msimu katika ukanda wa pwani. Migandamizo mikubwa ya hewa iliyopo kusini mwa Afrika inatarajiwa kuimarika na hivyo kusababisha hali ya ubaridi katika maeneo mengi hapa nchini na vipindi vya upepo mkali.

HALI YA HEWA KWA KIPINDI CHA MWEZI JUNI, 2018
Katika kipindi cha mwezi Juni, 2018 hali ya joto la wastani hadi chini ya wastani inatarajiwa katika maeneo mengi ya nchi. Hata hivyo vipindi vya baridi vinatarajiwa hususan nyakati za usiku na alfajiri. Ufuatao ni mwelekeo wa hali ya hewa nchini;

Pwani ya kaskazini (Mikoa ya Tanga, Pwani, Dar es Salaam, Morogoro pamoja na visiwa vya Unguja na Pemba): Viwango vya chini vya joto vinatarajiwa kuwa kati ya nyuzi joto 12 hadi 20 katika maeneo mengi. Hata hivyo baadhi ya maeneo ya miinuko ya mkoa wa Tanga hususani wilaya za Lushoto na Bumbuli zinatarajiwa kuwa na kiwango cha chini ya nyuzi joto 12. Hali ya ukavu kwa ujumla pamoja na vipindi kadhaa vya mvua za nje ya msimu inatarajiwa hususan katika kumi la pili la mwezi Juni, 2018.

Nyanda za juu kaskazini mashariki (Mikoa ya Kilimanjaro, Arusha na Manyara): Viwango vya chini vya joto vinatarajiwa kuwa kati ya nyuzi joto 8 hadi 12 katika maeneo mengi. Haya hivyo baadhi ya maeneo ya miinuko yanatarajiwa kuwa na kiwango vya chini ya nyuzi joto 8. Hali ya ukavu kwa ujumla inatarajiwa.

Kanda ya ziwa Victoria (Mikoa ya Kagera, Geita, Shinyanga, Mwanza, Mara na Simiyu): Viwango vya chini vya joto vinatarajiwa kuwa kati ya nyuzi joto 8 hadi 15 katika maeneo mengi. Haya hivyo maeneo ya miinuko ya mikoa ya Kagera na Geita yanatarajiwa kuwa na kiwango vya chini ya nyuzi
joto 8. Hali ya ukavu kwa ujumla inatarajiwa.

Magharibi mwa nchi (Mikoa ya Kigoma, Katavi na Tabora): Viwango vya chini vya joto vinatarajiwa kuwa kati ya nyuzi joto 10 hadi 14 katika maeneo mengi. Hali ya ukavu inatarajiwa.
Kanda ya kati (Mikoa ya Dodoma na Singida): Viwango vya chini vya joto vinatarajiwa kuwa kati ya nyuzi joto 8 hadi 14 katika maeneo mengi. Hali ya ukavu inatarajiwa.

Nyanda za juu kusini magharibi (Mikoa ya Rukwa, Njombe, Iringa na Mbeya): Viwango vya chini vya joto vinatarajiwa kuwa kati ya nyuzi joto 4 hadi 12 katika maeneo mengi. Hata hivyo maeneo ya miinuko pamoja na mkoa wa Njombe yanatarajiwa kuwa na kiwango cha chini ya nyuzi joto 4.
Maeneo ya kusini mwa mkoa wa Morogoro yanatarajiwa kuwa na kiwango cha chini cha joto cha juu ya nyuzi joto 12. Hali ya ukavu inatarajiwa kuendelea katika maeneo mengi, ingawa kuna uwezekano wa vipindi vichache vya mvua hususan katika maeneo ya miinuko (Tukuyu na Njombe).

Pwani ya kusini (Mikoa ya Mtwara na Lindi): Viwango vya chini vya joto vinatarajiwa kuwa kati ya nyuzi joto 12 hadi 18 katika maeneo mengi. Hali ya ukavu inatarajiwa kuendelea.

Kanda ya kusini (Mkoa wa Ruvuma): Viwango vya chini vya joto vinatarajiwa kuwa kati ya nyuzi joto 8 hadi 14 katika maeneo mengi. Maeneo ya miinuko ya mkoa wa Ruvuma yanatarajia kupata chini ya nyuzi joto 8 katika kipindi cha mwezi Juni, 2018.Hali ya ukavu inatarajiwa kuendelea.

Imetolewa na;
MAMLAKA YA HALI YA HEWA TANZANIA

Jumanne, 5 Juni 2018

LEO NI SIKU YA MAZINGIRA DUNIANI


Leo ni siku ya MAZINGIRA DUNIANI. Siku ya Mazingira Duniani huazimishwa duniani kote kila mwaka, tarehe 5 mwezi wa Sita. Lengo la siku hii ni
Kauli mbiu ya Kimataifa ya mwaka huu 2018 kidunia inasema “KOMESHA UCHAFUZI WA MAZINGIRA UTOKANAO NA PLASTIKI” Leo la kauli mbiu hii ni kuhamasisha watu wote kuachana na matumizi holela la plastiki yanayosababisha uchafuzi wa mazingira ikiwemo ardhi, hewa na vyanzo vya maji kama maziwa na bahari. Uzalishaji na matumizi ya kupindukia ya vifaa vya plastiki huathiri mazingira na bayoanuai na viumbe akiwemo mwanadamu. Hivyo dunia anahamasishwa kuwa na harakati endelevu za kulinda maisha ya viumbe na maliasili ili kuifanya dunia kuwa safi na yenye mazingira bora kwa kutokuwa na uchafuzi wa hewa, ardhi, na ,maji utokanao na matumizi holela ya vifaa vya plastiki. Kidunia maadhimisho ya siku hii ya Mazingira Duniani yatafanyika nchini India. India imechaguliwa na Umoja wa Kimataifa kutokana na harakati za muda mrefu za nchi hiyo katika kupambana na matumizi holela ya plastiki. Kwa hivi sasa nchi ya India imeonyesha uongozi bora katika kukabili mabadiliko ya tabia nchi na ni nchi yenye mikakati thabiti ya kuhamia kwenye uchumi utoao kiwango kidogo cha hewa ukaa.
Siku ya Mazingira Duniani ilianza kuadhimishwa mwaka 1972 na sasa imekuwa ni maadhimisho ya kimataifa yenye lengo la kuelimisha umma kuhusu masuala mbalimbali yahusuyo mazingira.
Nchini Tanzania Kauli mbiu ya mwaka huu ni “MKAA NI GHARAMA, TUMIA NISHATI MBADALA. Serikali ya jamhuri ya Muungano wa Tanzania imeweka kauli mbiu hii kutokana na kiasi kikubwa cha maeneo ya Misitu yanayoharibiwa kwa ajili ya kupata mkaa. Takwimu zinaonyesha hadi kufikia mwaka jana (2017) kiasi cha hekta 46,942 huharibiwa kila mwaka. Uharibifu wa misitu unasababisha uwepo wa changamoto za kimazingira kama vile ukosefu wa mvua unaoleta ukame;  hali ya jangwa na joto; upotevu wa viumbe hai mbalimbali na mimea ya asili; uharibifu wa vyanzo vya maji na uchafuzi wa ardhi

Kauli mbiu yetu

BUFADESO kwa maendeleo ya wakulima

MUHIMU

Makala na picha zinazochapishwa katika blogu hii ni kwa ajili ya taarifa na kumbukumbu za Shirika la Bunda Farmers Development Support Organization (BUFADESO)
Hairuhusiwi kutumia yaliyomo katika blogu hii (HASA PICHA) kwa shughuli zozote bila ruhusa ya mmiliki wa blogu hii ambaye ni BUFADESO